Na. Jacob Kasiri -Mbeya.
Ikiwa zimebaki takribani siku 4 zoezi la *VoteNow* lihitimishwe rasmi Mei 04, 2025 saa 6:00 usiku, kampeni hiyo imepata hamasa baada ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Prof. Aloys Mvuma kushiriki zoezi la kuzipigia kura Hifadhi za Taifa 10 zilizoingia katika kinyang’anyiro cha Tuzo za World Travel Awards na kuwahimiza Wanazuoni wenzake na Wanafunzi kushiriki zoezi hilo ili tuzo hizo zirejee Tanzania.
Akiwa katika zoezi la kupiga kura Prof. Mvuma alisema,”Nina imani TANAPA mtashinda kwani rasilimali zenu zimetunzika vizuri mathalani, mazingira na baianoai zimeendelea kuongezeka na kushamiri pia, maeneo yenu ya Hifadhi za Taifa tumeendelea kuyatumia kwa ajili ya tafiti zetu na mafunzo kwa vitendo kwa ajili ya wanafunzi wetu kutokana na ubora wa maeneo hayo.”
Aidha, Prof. Mvuma aliongeza kuwa tumeona jitihada kubwa alizozifanya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuvitangaza vivutio vyetu kupitia Filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania, hivyo nasi tuungane naye kwa kuzipigia kura na kuzitembelea hifadhi hizo ili tuchangie pato la Taifa kupitia utalii.
Sanjari na kupiga kura pia Prof. Mvuma ameahidi kutembelea Hifadhi ya Taifa Kitulo akiongozana na wanazuoni wenzake pamoja na watumishi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ili kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika hifadhi hiyo inayosifika kwa maua aina ya Chikanda.
Akitoa maelekezo ya namna ya kupiga kura kiongozi wa jopo la Maafisa na Askari kutoka TANAPA wanaoongoza zoezi hilo Afisa Mwandami Richard Hayri alisema kuwa lengo ni kuwahamasisha watanzania wengi ili wapige kura kwani ushindi wa TANAPA ni ushindi kwa Taifa.
Mwandamizi Hayri aliongeza, “Tukishinda tutaongeza wigo wa uelewa na imani kwa watalii kuhusu nchi, vivutio pamoja na watu wake. Kama ilivyozoeleka watanzania wanasifika kwa ukarimu, tamaduni mbalimbali, chakula mchanganyiko, ngoma na mavazi ya asili ambayo yameendelea kuvutia watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali, sifa hizi na ushindi tutakaopata utaongeza idadi ya watalii watakaotembelea hifadhi zetu na kuliongezea taifa mapato na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa watakaowekeza katika malazi, kilimo, vinyago, usafirishaji na sekta ya afya”.
Kutokana na hamasa iliyochagizwa na Profesa Aloys Mvuma – Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya leo Aprili 30, 2025 takribani kura 621 zimepigwa zikiwahusisha Wanazuoni, Wafanyakazi na Wanafunzi wa chuo hicho.