Na WAF – Handeni, Tanga.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewataka wamiliki wa vyuo vya afya nchini kudahili idadi ya wanafunzi kulingana na uwezo wa chuo ikiwemo miundombinu ya darasani pamoja na kwenye maabara za mafunzo kwa vitendo ili kuwa na ubora wa elimu kwa vyuo hivyo.
Waziri Mhagama amesema hayo leo Mei 2, 2025 akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango kwenye hafla ya mapokezi ya Chuo Cha Afya cha Mafunzo ya Taaluma ya Uuguzi na Ukunga kilichofadhiliwa na Shirika la Hisani la Sheikh Abadallah Alnouri kutoka nchini Kuwait kilichojengwa wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.
“Tunaendelea kutoa angalizo kwa vyuo vyote vya afya nchini, pale vyuo vyetu vinapoanza kutoa mafunzo ni lazima vihakikishe vinakuwa na maabara za kujifunzia kwa vitendo kabla mwananfunzi hajaenda kumhudumia mgonjwa ili kujiimarisha kwenye mafunzo,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amevitaka vyuo hivyo kupata hospitali kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo inayotosheleza mahitaji ikiwa ni pamoja na Chuo cha Afya cha Mafunzo ya Taaluma ya Uuguzi na Ukunga walichokipokea leo ambacho kipo karibu na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ili wanafunzi waweze kufika katika hospitali hizo ambazo wanaweza kujijengea uwezo.
Vilevile, Waziri Mhagama amewataka wamiliki, wakufunzi na wanafunzi kuendelea kusimamia maadili na miiko inayotakiwa kuzingatiwa wakati wa mafunzo ya Sekta ya Afya pamoja na wakati wa utendaji kazi kama watumishi wa afya ili kuifamya Sekta ya Afya kuendelea kutoa mchango unaohitajika katika ujenzi na uimara wa Taifa.
“Leo kwa heshima kubwa tunakubaliana kuwa, tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo yao, hivyo Serikali itaendelea kufanya kila liwezekanalo kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini,” amesema Waziri Mhagama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Buriani amesema mkoa huo umepokea jumla ya Shilingi Bilioni 72 za kuboresha huduma za afya ikiwemo ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali pamoja na ununuzi wa vifaa tiba na dawa.
“Lakini pia katika mkoa wetu Mhe. Waziri tumefanikiwa kupunguza vifo vya kina mama wajawazito kutoka vifo 55 katika kila vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2021 hadi kufikia vifo 30 katika kila vizazi hali 100,000 kwa mwaka 2024,” amesema Dkt. Batilda.
Naye, Mwenyekiti wa Sheikh Alnouri Charity Organization Bw. Jamal Alnouri amesema kwa kushirikiana na Serikali ya Kuwait wataendelea kutoa msaada kwa Serikali ya Tanzania hasa katika Sekta ya Afya kwakuwa afya ni suala la msingi katika maendeleo