Shirika la umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Ruvuma, limewataka wafanyakazi wa Shirika hilo kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme nyakati zote kwani hitaji lao ni umeme na nasio maneno.
Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Boniface Malibe, wakati wa hafla iliyoandaliwa na Afisa Rasilimaliwatu wa Shirika hilo ya kuwapongeza wafanyakazi bora iliyofanyika katika ukumbi Hertage Cortege Mjini Songea ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani.
Mhandisi Malibe amesema kwasasa wamefanikiwa kuondoa changamoto ya kukatikakatika kwa umeme ukilinganisha na kipindi cha nyuma ikiwa ni moja ya hatua kubwa inayofanywa na shirika hilo katika kuboresha huduma hiyo muhimu inayotegemewa na jamii kwenye kuchochea uchumi endelevu.
Amewashukuru wafanyakazi wote kwa ujumla kwa ushirikianao mkubwa wanao uonyesha huku rai yake kwao ni kuhakikisha kila mteja anae ripoti tatizo au changamoto anapata huduma ndani ya dakika 30 changamoto yake iwe imekwisha tatuliwa.
Wakizungumza baadhi ya wafanyakazi wamepongeza jitihada za shirika hilo katika kuleta hamasa kwa wafanyakazi kwa kuandaa hafla mbalimbali za kuwakutanisha pamoja kwa kutoa motisha na zawadi ili kuongeza uchapakazi wa watumishi.
TANESCO Ruvuma imetoa zawadi mbalimbali kwa wafanyakazi wa Kudumu na wale wa Miktaba pamoja na kuzizawadia Wilaya zote TV za kisasa kutokana na utendaji mzuri wa kazi.
Maadhimisho ya Siku wafanyakazi Duniani kitaifa yalifanyika Mkoani Singida, ambapo kwa Mkoa wa Ruvuma yaliadhimishwa katika Manispaa ya Songea chini ya kauli mbiu isemayo “Uchaguzi Mkuu wa 2025, utuletee viongozi wanaojali na kuthamini haki na maslahi ya wafanyakazi, Sote tushiriki “.