Na Mwandishi Wetu
WADAU wa zao la Mpunga nchini wametakiwa kuzichangamkia fursa zipatikanazo kwenye mnyororo mzima wa thamani kwenye zao la mpunga.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar wakati akifunga Mkutano wa Kitaifa wa Wadau wa Zao la Mpunga uliofanyika Hoteli ya St. Gasper Jijini Dodoma, tarehe 24 Aprili 2025.
Dk. Omar amesema kuwa kutoka na fursa lukuki kwenye zao hilo wananchi wa sehemu mbalimbali linapolimwa wameinuka kimaisha kutokana na mauzo ya zao hilo.
Pia Dk. Omar amebainisha kuwa zao la mpunga ni zao la pili linalokua kwa kasi nchini huku uzalishaji wake umeongezeka kwa asilimia 5 kutoka mwaka 2010.
Amebainisha kuwa tija ya zao hilo inatarajiwa kuongezeka kutoka tani 2 kwa hekta kufikia tani 4.4 kwa hekta katika kilimo cha mvua na tani 7.34 kwa hekta katika kilimo cha umwagiliaji.
Pia Dkt. Omar ameshukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupandisha bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka shilingi Bilioni 294.16 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia shilingi Trilioni 1.249 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo ongezeko hilo la bajeti ya Wizara inachangia kuongezeka kwa tija katika uzalishaji wa zao la mpunga.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi – Uchumi na Uzalishaji katika Mkoa wa Morogoro, Dkt. Rozalia Rwegasira ameshauri wakulima wa zao la mpunga kutumia zaidi kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa zao hilo na watumie mbegu bora zenye kuhimili mabadiliko ya tabianchi ili kuongeza zaidi tija na uzalishaji.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi – Uchumi na Uzalishaji katika Mkoa wa Tabora, Bw. Abrahaman Mndeme amesema lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga kutoka tani Milioni 4 za sasa na kufikia tani milioni 7 ifikapo 2030.
Aidha, Mwakilishi wa Kampuni ya Japan International Cooperation Agency (JICA) Tanzania, Bw. Ara Hitoshi amesema ushindani kwenye uzalishaji wa zao la mpunga unaongezeka na mkutano wa wadau wa zao la mpunga utasaidia kufanikisha azima ya Serikali ya kukuza zaidi kilimo cha zao la mpunga.
Mkutano huo wenye Kauli mbiu isemayo “Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo na matokeo chanya ya Tasnia ya Mpunga”, umehudhuriwa na Wakurugenzi wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo.
Pia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda na Biashara, Makatibu Tawala Uchumi na Uzalishaji wa mikoa ya Mbeya, Shinyanga, Katavi, Tabora na Morogoro, Wasindikaji na Wakulima kutoka maeneo yanayozalisha kwa wingi zao la mpunga hapa nchini.