Muonekano wa Bweni katika Shule ya Sekondari Nyasa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma lenye uwezo wa kuchukua Wanafunzi 80.
Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyasa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma, wakiwa mbele ya Bweni lao.
……………..
Na Mwandishi Maalum,
Mbambabay
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Nyasa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kuwajenga Bweni ambalo limewasaidia kupata muda mwingi wa kujisomea na kukomesha vitendo vya kikatili wanapotoka shule na kurudi nyumbani.
Wakizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzao wamesema,awali changamoto ya bweni iliwakosesha kupata muda wa kujisomea masomo ya ziada baada ya muda wa kawaida,kwani hata wanapofika nyumbani walitumia muda huo kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kupika na kuchota maji.
Judith Mapunda mwanafunzi wa kidato cha tano alisema,kujengwa kwa bweni katika shule hiyo kutasaidia kufanya vizuri kimasomo kwa kuwa watatumia muda wa ziada wa kujisomea na kukumbuka yale waliyofundishwa na walimu wao.
Aidha Mapunda alisema,bweni hilo limewahakikishia usalama wao dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia wanaporudi nyumbani nyakati za jioni kwani walikuwa wanakutana na matukio mabaya njiani ikiwemo kubakwa na wauni hasa vijana wanaofanya shughuli za boda boda.
Alisema,kujengwa kwa bweni hilo kutapunguza utoro na visababishi vya mimba vinavyotokana na vishawishi vya barabarani wakati wa kwenda na kutoka shule na kuiomba Serikali kuwajengea uzio ili kuzunguka bweni hilo.
Nathaniel Agostino alisema,kabla ya kujengewa bweni walilazimika kulala watu wawili kitanda kimoja hivyo kupelekea kupata magonjwa ya kuambukiza, lakini sasa magonjwa hayo yamepungua kwa kuwa kila mwanafunzi analala kwenye kitanda chake.
Ameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kujenga bweni ambalo lina miundombinu rafiki na mizuri inayohamasisha wanafunzi kupenda kuishi bweni na kuhamasisha kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao.
Mkuu wa shule hiyo Nonoso Mtweve alisema,bweni hilo ni sehemu ya uboreshaji wa miundombinu katika shule hiyo inayofanywa na Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya Nyasa ili kuwawezesha wanafunzi hasa wasichana kupata haki yao ya kupata elimu bora na kuwapa mazingira salama ya kufikia ndoto zao.
Alisema,ujenzi bweni hilo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 limetatua changamoto ya wanafunzi wa kike waliokuwa wakitembea umbali mrefu na kupunguza tatizo la utoro wa reja reja na kuongeza ari ya wanafunzi wa shule hiyo kujisomea.
Alisema, bweni hilo limegharimu jumla ya Sh.milioni 123 na zimebaki Sh.mlioni 6 ambazo wameomba kufanya ukarabati wa baadhi ya majengo chakavu yaliyopo ili wanafunzi na walimu wapate sehemu nzuri na salama ya kujifunzia na kufundishia.
Mtweve alisema,kupitia bweni hilo wamepata mafanikio mengi ikiwemo kupunguza umbali kwa wanafunzi wakati wa kwenda na kurudi shule kwani wapo waliokuwa wanaishi umbali wa kilometa zaidi ya 20 ambao sasa wanaishi shuleni na kuwahi vipindi vya masomo darasani.
Alitaja mafanikio mengine ni kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi wanaochaguliwa kuendelea na kidato cha tano ikilinganishwa na miaka ya nyuma,kupungua kwa utoro,mimba kwa wanafunzi wa kike na limehamasisha wanafunzi wengi kupenda kwenda shule.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Khalid Khalif alisema,katika kipindi cha miaka minne cha Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wamepokea zaidi ya Sh.bilioni 5.89 kati ya hizo Sh.bilioni 2.1 zimekwenda katika sekta elimu.
Alisema,fedha hizo zimetumika kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya elimu majengo ya madarasa,matundu ya vyoo,mabweni na majengo mengine yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nyasa.
Alisema,Halmashauri ya Wilaya Nyasa ina Shule za Sekondari 23 zenye jumla ya wanafunzi 9,339 na kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wamepokea Sh.milioni 397 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kwenye shule 4 za sekondari ikiwemo shule ya Nyasa.
Alieleza kuwa,uwepo wa mabweni umetatua changamoto nyingi ikiwemo kupunguza umbali kwa watoto kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni,kupunguza mdondoko na kutojiingiza kwenye vitendo vya ovyo ikiwemo mimba kwa wasichana na ulevi kwa wavulana.
“Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa tuna jumla ya mabweni 19 na mahitaji yetu ni mabweni 71 hivyo bado tuna mahitaji makubwa,upungufu wa mabweni katika shule zetu kuna athiri sana mahudhurio ya watoto shuleni na kupelekea utoro na kusababisha ufaulu mdogo kwa wanafunzi wa kidato cha pili na nne”alisema.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Nyasa iliyowezesha kuboresha maisha ya Wananchi na watumishi wa umma kupata sehemu nzuri ya kufanyia kazi.