


Baadhi ya Wanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mkali Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma wakiwa Darasani,Serikali kwa kushirikiana na Wazazi imefanikiwa kujenga jumla ya vyumba sita vya madarasa katika shule hiyo ili kuwanusuru wanafunzi wanaotoka kata ya Mkali kutembea zaidi ya kilometa sita kwenda kata ya Liuli na Lundo kufuata masomo.
…………………
Na Mwandishi wetu,
Nyasa
BAADHI ya Wazazi wa Kijiji cha Mkali Kata ya Mkali Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kutekeleza mradi wa shule mpya ya Sekondari ambayo imemaliza mateso ya muda mrefu kwa watoto wao kutembea umbali zaidi ya kilometa sita kwenda kata za jirani kwa ajili ya kufuata masomo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa kiijiji hicho walisema,shule hiyo imesaidia watoto wa kijiji hicho ambao awali walilazimika kwenda Shule ya Sekondari St Paul Liuli umbali wa kilometa sita na shule ya Sekondari Lundo iliyopo umbali wa wa kilometa tano.
Isac Mkwera alisema,mradi huo umeibuliwa na wazazi wenyewe baada ya kuona mateso wanayopata watoto wao kwenda maeneo mengine kufuata masomo na walianza kuchangishana Sh.3,000 kwa kila kaya ambazo zilizowezesha kufyatua tofali na kununua saruji.
Mkwera alisema,walifanikiwa kujenga boma na Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya Nyasa imewasaidia kupiga kenji,misumari,kutoa bati na rangi ambazo zimewezesha kukamilisha vyumba sita vya madarasa.
Mkwera,ameiomba Serikali kuongeza vyumba vya madarasa ili vijana wengi wanaomaliza darasa la saba katika kijiji hicho wapate nafasi ya kuendelea na elimu ya Sekondari katika shule hiyo kwani madarasa yaliyopo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi wachache.
Eveline Chiwinga alisema,kujengwa kwa shule hiyo kumepunguza sana matukio ya uhalifu na wahalifu kwani vijana wanapomaliza darasa la saba wanapata nafasi ya kuendelea na elimu ya Sekondari.
Alisema,awali baadhi ya vijana ambao hawakupata nafasi ya kujiunga na Sekondari walishinda vijiweni na wengine kujiingiza kwenye matukio ya uharifu kama wizi na kuvuta bangi.
William Mbunda,ameiomba Serikali kupeleka miundombinu ya maji,umeme na kuboresha barabara ili watoto na walimu waweze kufika shuleni kwa urahisi kutokana na barabara inayokwenda shuleni kuwa makolongo mengi na mifereji inayojaa maji hasa wakati huu wa masika.
Akizungumza kwa niaba ya Wanafunzi wenzake Janeth Mahai,ameishukuru Halmashauri ya Wilaya Nyasa kwa kutoa fedha za kujenga vyumba sita vya madarasa na matundu ya vyoo.
Alisema,shule hiyo ni ukombozi mkubwa kwao siyo kwa ajili ya kupata elimu tu bali imewasaidia kuepukakana na vitendo vya kikatili vilivyofanywa na vijana hasa boda boda ambao walitumia nafasi ya kuwata lifti kuwafanyia vitendo vya kiuni ikiwemo kuwabaka na kuwapa mimba.
Ameiomba Serikali,kuwapelekea umeme utakowezesha kusoma masomo ya Sayansi yanayohitaji sana elimu kwa vitendo ili waweze kufanya vizuri na kutimiza ndoto walizonazo.
Mkuu wa Shule hiyo Constatino Haule alisema,ujenzi wa shule hiyo ulianza mwaka 20222 kwa nguvu za Wananchi na kukamilika mwaka 2024 baada ya Serikali kutoa kiasi cha Sh.milioni 108.
Alisema,kati ya fedha hizo Sh.milioni 50 zimetumika kukamilisha vyumba vinne vya madarasa,Sh.milioni 10 kwa ajili ya kujenga matundu 10 ya vyoo na Sh.milioni 48 kujenga vyumba viwili ambavyo ujenzi wake uko hatua ya mwisho kukamilika.
Hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo umegharimu Sh.milioni 87,645,496 kati ya Sh.milioni 108 na fedha hizo zimetumika kununua vifaa vya ujenzi na malipo ya fundi.
Kwa mujibu wa Mwalimu Haule,mradi huo umefikia hatua ya mwisho na kazi zilizobaki ni uwekaji wa waya wa mbu na kufunga vioo madirishani na kwa upande wa vyoo wako hatua ya mwisho kukamilisha ambapo kazi zilizobaki ni kujenga kichomea taka,ujenzi wa chemba za maji na ujenzi wa tenki la maji.
Ameishukuru Serikali,kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa shule hiyo kwani imesaidia sana kuwapunguzia watoto wanaotoka eneo hilo kutembea umbali mrefu kwenda maeneo mengine kufuata masomo,kupunguza tatizo la utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike.