Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ambaye ndiye mwandaaji wa jukwaa hilo, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi badala ya kuwa wasikilizaji tu wa mijadala ya kitaalamu.
“Haipaswi tu kuwa wasikilizaji wa mada, bali wachukua hatua,” alisema.
Makonda alieleza kuwa jukwaa hilo lina lengo la kuwasaidia wananchi kupata uelewa wa kina kuhusu namna ya kuwekeza katika sekta zinazokua kwa kasi kama utalii, kilimo, biashara, na miundombinu.
“Tunaomba viongozi na wataalam waliokuja hapa watuambie tukitoka hapa fedha zinapatikanaje na wananchi wawekeze fedha zao wapi ili wasipate hasara,” alisema.
Akizungumzia mashindano ya AFCON yatakayofanyika Arusha, Makonda alitaja tukio hilo kama fursa adhimu kwa Watanzania.
“Mbali na kushangilia mpira, ni vyema kujua Watanzania watanufaika vipi kiuchumi,” alisema.
Katika mchango wake, Mwanamajumui mashuhuri wa Afrika, Profesa Patrick Lumumba, alipongeza hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuwakutanisha wadau wa sekta mbalimbali kujadili maendeleo ya kiuchumi.
“Naipongeza Arusha kwa kuwakutanisha wataalam mbalimbali kwa ajili ya kujadili fursa za kiuchumi. Tanzania sasa imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kisekta, ikiwemo sekta ya kilimo, madini, utalii pamoja na mahusiano ya kimataifa,” alisema Profesa Lumumba.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Seleman Jafo, alisisitiza umuhimu wa kujituma katika kazi ili kuonyesha fursa kwa vijana na kuharakisha maendeleo ya taifa.
“Niwaombe wana Arusha, ninyi mmeonyesha tofauti, songeni mbele msirudi nyuma.
Na kwenye hili, Mkuu wa Mkoa, itisha wakuu wengine wa mikoa, madiwani na viongozi wengine waje wajifunze. Wakija watalala hapa, mtapiga hela, mambo yataendelea,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, alisisitiza wajibu wa kila mkoa kubainisha fursa zilizopo ili wananchi waweze kuzitumia kwa manufaa ya kiuchumi.
“Ni wajibu kila mkoa sasa kuanisha fursa zilizopo kwenye mikoa yao, kufanya makongamano kama hili ili wananchi waweze kujua fursa zinazopatikana kwenye maeneo yao,” amesema.
Aidha Jukwaa hilo limejumuisha zaidi ya washiriki 1,000 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo mawaziri, wawekezaji, watunga sera na wajasiriamali. Lengo kuu likiwa ni kuwajengea uwezo wakazi wa Arusha kutumia mbinu sahihi za kuwekeza na kunufaika na fursa zilizopo kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.