Na Silivia Amandius.
Bukoba, Kagera.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amefanya ziara katika Tarafa ya Katerero, Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Kemondo-Maruku unaogharimu Shilingi Bilioni 15.8. Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia RUWASA, unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 100,000 kutoka Kata saba za Wilaya ya Bukoba Vijijini.
Mradi huu unaochukua maji kutoka Ziwa Victoria tayari umeanza kuhudumia Kata za Kemondo na Bujugo, huku maandalizi yakiendelea ili kusambaza huduma kwa Kata za Katerero, Kanyengereko, Maruku, Muhutwe na Mayondwe.
Akiwa katika eneo la mradi, Naibu Waziri Kundo alikagua miundombinu mbalimbali ikiwemo pampu mbili kubwa za kisasa zinazochota maji kutoka Ziwa Victoria, na tenki kubwa la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita milioni 3 ambalo limekamilika kwa asilimia 100. Alisisitiza kuwa mradi huu ni sehemu ya dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa ukaribu.
“Mradi huu ni kielelezo cha juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia katika kuimarisha huduma ya maji vijijini na kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake ya msingi ya maji,” alisema Naibu Waziri Kundo.
Mradi wa Kemondo-Maruku ulianza kutekelezwa baada ya kuwasilishwa na Mbunge wa Bukoba Vijijini, Mhe. Jasson Rweikiza, kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, na sasa umekamilishwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima na Kamati yake ya Usalama, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bukoba Vijijini Bi. Fatina Laay, Maafisa kutoka RUWASA na BUWASA, pamoja na viongozi wa Chama na Serikali wa ngazi ya Kata akiwemo Diwani wa Kata ya Kemondo, Ndugu Khatwibu Kahyoza.
Serikali inaendelea kutekeleza miradi mingi ya maji nchi nzima kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wananchi, kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya kweli kwenye jamii.