Na Janeth Raphael MichuziTv – Bungeni Dodoma
MBUNGE wa Kilindi Omary Kigua (CCM) ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kusimamia ujenzi wa barabara ya Handeni-Kibrash -Singida kwani ni muhimu kiuchumi na inaunganisha mikoa mitano.
Akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025-2026 bungeni,Kigua amesema yale ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati akizindua bandari ya Tanga hivyo ni lazima Waziri na timu yake wahakikishe barabara hiyo inakamilika.
“Ni barabara yenye uhitaji mkubwa kwa sasa hivi haipitiki mikoa yote ya Kaskazini inategemea barabara hii hebu nakuomba mheshimiwa Waziri yasibaki maneno tu ijengeni iweze kupitika,”amesema Kigua.
Pia ameiomba Wizara ya Ujenzi kuangalia barabara ya Chalinze- Segera ambapo amedai ilijengwa miaka ya 80 na siku za hivi karibuni zimekuuwa zikitokea ajali nyingi kutokana na uchakavu pamoja na ufinyu wa barabara hiyo.
“Nimuombe Waziri wa Ujenzi KM 20 kuanzia Handeni kwa kweli zinasua sua hebu msimamieni yule mkandarasi ambaye hayupo kazini sisi ndio tunamdai kazi ninauhakika wewe na timu yako mnaweza kumsimamia wananchi wanaihitaji ile barabara,”amesema Mbunge huyo.
Aidha Mbunge huyo pia amekumbusha madeni ya wakandarasi yalipwe kwa wakati ili waweze kuendelea na kazi kwani baadhi wamekuwa wakidai fedha nyingi.