NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka wananchi kuacha shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira zikiwemo kukata miti ovyo.
Ametoa wito huo bungeni jijini Dodoma leo tarehe 6 Mei, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Jacqueline Msongozi aliyetaka kufahamu Serikali imejipangaje katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanachangia uharibifu wa mazingira.
Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Khamis alisema pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali za kuhifadhi mazingira, wananchi wanapaswa kuepuka kilimo kisicho endelevu katika vyanzo vya maji, ufugaji unaochangia uharibifu wa mazingira na uvuvi haramu.
Aidha, Mhe. Khamis alisema katika kutekeleza maelekezo ya Serikali ni wajibu wa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku kuachana na matumizi ya nishati ya kuni na mkaa na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuchangia katika utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliandaa Sera, Mikakati, Kanuni, Miongozo na Mipango ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Alitaja mikakati hiyo kuwa ni Sera ya Taifa ya Mazingira (2021), Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026), Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022–2032) na Kanuni za Marekebisho ya Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni za mwaka 2023 ambazo zinasomwa pamoja na Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni za mwaka 2022.
Akijibu swali la nyongeza la mbunge huyo kuhusu Serikali imejipangaje kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira na kutoa miche bure kwa wananchi, Mhe. Khamis alisema mipango ya utoaji wa elimu ni endelevu.
Alifafanua kuwa wananchi wameendelea kuelimishwa kuhusu usimamizi wa taka na kutambua kuwa taka hizo ni fursa wazitumie kujipatia kipato kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali badala ya kuziacha zikizagaa ovyo.
Sanjari na hilo, pia Naibu Waziri alisema kuwa katika kuhakikisha wananchi hawafanyi shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji, wanaelimishwa kuhusu Sheria ya Mita 60 ambayo inawataka waache kufanya shughuli hizo ndani ya eneo hilo.
”Tumeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kulinda fukwe kwani sote tunatambua kuna changamoto katika baadhi ya visiwa kuliwa na maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi hivyo tunawaelimisha wapande miti katika fukwe hizo ili kuziimarisha,” alisema.
Aliongeza kuwa ipo mikakati ya Serikali ya kushirikiana na wadau wanazolisha miche kuona namna ya kuigawa bure kwa wananchi ili kila mmoja ashiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji wa miti na kuitunza.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiteta jambo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga wakati Kikao cha 18 Mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 06 Mei, 2025. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga na mbele ni Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa.