
Katika mwalo wa Makatani, kata ya Nkome wilayani Geita, mwanamke mmoja jasiri, Pili Wambura, ameibuka kama mfano wa kuigwa kwa wanawake waliovunja vikwazo vya kijinsia kwa kujitosa katika kazi ya upakaji rangi kwenye mitumbwi ya wavuvi – kazi ambayo kwa muda mrefu imeonekana kuwa ya wanaume.
Akizungumza na muandishi wetu akiwa kazini mwaloni, Pili alisema alijifunza kazi hiyo kutoka kwa mumewe, Masumbuko Muga, ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika fani hiyo. Kwa sasa, anasema kazi hiyo si tu imemwezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya familia yao, bali pia imempa uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
“Awali nilitegemea kila kitu kutoka kwa mume wangu, lakini sasa najitegemea. Tunashirikiana kutatua changamoto za familia kama washirika sawa,” alisema Pili huku akipaka rangi kwenye mtumbwi mmoja.
Kwa upande wake, Masumbuko alisema aliamua kumfundisha mke wake kazi hiyo kutokana na mapenzi aliyonayo kwake na kutaka kumjengea uwezo wa kiuchumi. Hadithi yao imekuwa chanzo cha msukumo kwa wanandoa wengine katika jamii hiyo, wakithibitisha kuwa mafanikio ya kifamilia yanawezekana pale wawili wanaposhirikiana kwa dhati – bila kujali kazi inachukuliwa vipi na jamii.