Serikali mkoani Mara imekabidhi hati mbili za shamba la umwagiliaji la Bugwema lililopo katika halmashauri ya Musoma vijijini kwa Tume ya Taifa ya Umwagilaiji.
Mashamba hayo ni maalumu kwaajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu ya shamba hilo ili liweze kutumika kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Shamba hilo ni miongoni mwa mashamba matano ya mfano yanayotarajiwa kuanzishwa na Tume hiyo hapa nchini kwaajili ya kuboresha na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji.
Akikabidhi hati hizo leo Jumatano Mei 7,2025, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya ameiomba Tume hiyo kuhakiksha shamba hilo linaanza uzalishaji haraka ili kuwanufaisha wakazi wa eneo hilo na mkoa kwa ujumla.
Alisema Shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 3,000 limekaa kwa muda mrefu bila kufanyakazi.
“Tayari tumekamilisha suala la umiliki wake tunaomba Tume ihakikishe uzaliahaji unaanza mapema ili kuwanufaisha wananchi wa maenoe yale na watanzania kwa ujumla,” amesisitiza.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa akizungumza mara baada ya kupokea hati hizo amesema ujenzi wa miundombinu ya shamba hilo unatarajiwa kuanza kujengwa ndani ya wiki mbili zijazo.
Kwa mujibu wa Mndolwa, Serikali inalenga kulifanya shamba hilo pamoja na mengine manne kuwa ya mfano ili kuboresha kilimo cha umwaguliaji hapa nchini kutokana na umuhimu wa kikimhicho katika kukuza na kufanya sekta ya kilimo kuwa endelevu
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya shamba hilo kutakuwa na utaratibu maalum wa kulima ambapo wakazi wa maeneo hayo watapewa kipaumbele sambamba na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
“Tukikamlisha ujenzi wa miundombinu tutakuwa na makundi mawili ya wakulima pale kwa maana wananchi wa kawaida wenye uwezo wa kulima heka moja hadi tano pamoja na wawekezaji wa kulima heka tano na kuendelea, kutakuwa na mfumo maalum na rafiki ambao utawezesha lengo hili la serikali kufanikiwa,” amesisitiza
Mndolwa amefafanua kwamba, shamba hilo la Bugwema lilianzishwa mwaka 1974 na Raisa wa awamu ya kwanza hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere ambapo liliwekewa miundombinu kadhaa yakiwpeo mabomba lakini lilishindwa kuanza uzalishaji kutokana na sababu mbalimbali.
“Serikali ya awamu ya sita imeona kuna umuhimu wa kufufua shamba hili ili kuenzi maono ya Mwalimu lakini pia ikiwa ni njia mojawapo ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji kwaajili ya kuboresha kipato cha mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema
Ametaja mashamba mengjne yanayotarajiwa kuwa mashamba ya mfano kuwa ni pamoja na shmaba la Chinamgali lililopo Dodoma, Kibondo lililopo mkoani Kigoma,Mbarali na Madibila mkoani Mbeya.
Amesema mashamba hayo yatawekewa miundombinu ya kisasa ili kuwezesha kilimo cha kisasa ambacho kitafanyika kwa mwaka mzima na kwamba baada ya mashamba hayo Tume hiyo inatarajia kuendelea kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji katika maeneo mengine nchini ili kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.
Baadhi ya wakazi wa Musoma wameipongeza seeikali kwa hatua hiyo iliyofikiwa huku wakitaka ujenzi wa miundombinu hiyo kukamilika kwa haraka na hatimaye shamba liweze kuanza uzalishaji.
Mgosi Warioba amesema shamba hilo limekuwepo zaidi ya miaka 50 bila kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa hivyo uamuzi wa kulifanya shamba hilo kuwa la mfano ni wa kupongezwa.
“Eneo ni zuri sana lipo karibu na ziwa Victoria na mto Bugwema kwahiyo uhakika wa maji ni asilimia 100 wananchi tulikuwa tunasikitika eneo kukaa hivyo hivyo bila uzalishaji,niombe tu huu mchakato ukamilike haraka ili wengi waweze kunufaika,” amesema
Musa Amos amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi huo wakazi wa maeneo hayo wanastahili kupewa kipaumbele hatua ambayo mbali na kuimarisha uchumi wao pia itawasidia waweze kulima kisasa na kufaya kilimo chenye tija.Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya akikabidhi hati mbili za shamba la umwagiliaji la Bugwema lililopo katika halmashauri ya Musoma vijijini kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa