Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), leo 7/5/2025, imetoa semina ya Udhibiti katika utekelezaji wa miradi ya gesi ya kupikia, gesi asilia na CNG inayozalishwa nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ili wapate uelewa wa kina juu ya mwenendo na utendaji wa sekta hiyo yenye faida na manufaa kiuchumi nchini.
Akiwasilisha andiko lake, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, ameeleza kuongezeka kwa hali ya ushindani katika biashara ya LPG kwa kuongezeka kwa makampuni yanayofanya biashara hiyo hali inayopelekea kuongezeka wa watumiaji wa nishati hii safi.
Kwa upande wa gesi asilia, Dkt. Andilile alisema, EWURA imetoa leseni 11 za vituo na biashara ya CNG na vibali vya ujenzi 22 vya miradi ya vituo vya CNG na kwamba 78% ya gesi asilia inatumika kuendesha vyombo vya moto na 22% viwandani.
“EWURA inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya LPG na CNG, kulinda afya za wananchi kwa kuhakikisha wanatumia nishati safi, kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli na dizeli ambayo ni ghali na yenye madhara kwa mazingira kwa kuhamasisha matumizi CNG kwenye magari” alimalizia Dkt. Andilile.
Wengine waliofanya wasilisho ni pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ma Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakifuatilia kwa makini wasilisho hilo