Katika juhudi endelevu za kuboresha usimamizi wa kodi na kuongeza uzingatiaji miongoni mwa wazalishaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na SICPA Tanzania, wameanza mafunzo ya kitaifa kuhusu matumizi ya programu mpya ya simu ya Smart DAS (Huisha Kidijitali).
Juhudi hizi ni sehemu ya mkakati mpana wa kurahisisha mchakato wa kutangaza Stempu za Kielektroniki (ETS), kupunguza makosa ya kibinadamu na kuboresha ufanisi kwa walipa kodi pamoja na wasimamizi wa sheria za kodi.
Programu ya Smart DAS, ambayo sasa inapatikana kwenye mifumo ya Android na iOS, inaleta suluhisho la haraka kwa walipa kodi. Badala ya kuingiza namba za mfululizo wa stempu kwa mkono — mchakato uliokuwa unachukua muda na kuwa na uwezekano mkubwa wa makosa — wazalishaji sasa wanaweza kuchanganua (scan) stempu ya kwanza na ya mwisho katika kila kifurushi. Programu hiyo hukusanya taarifa zote muhimu moja kwa moja na kuziwasilisha kwenye mfumo wa kati wa TRA, hivyo kupunguza muda wa kutangaza na kuboresha usahihi wa taarifa.
“Programu hii ni jibu la moja kwa moja kwa mahitaji ya walipa kodi wetu,” alisema Bw. Abyud Tweve, Meneja wa Mradi wa ETS kutoka Idara ya Mapato ya Ndani Makao Makuu ya TRA. “Tulisikiliza changamoto zao na tumejibu kwa suluhisho la vitendo na rahisi kutumia ambalo sio tu linarahisisha uzingatiaji, bali pia linaimarisha uwezo wetu wa kusimamia na kuthibitisha uzalishaji katika muda halisi.”
Ili kuhakikisha utekelezaji mzuri wa programu hii, TRA iliandaa mafunzo maalum jijini Dar es Salaam ambayo yalihusisha maafisa 92 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Maafisa hao, ambao wanasimamia maeneo ya ETS na Vifaa vya Kielektroniki vya Kodi (EFD) katika mikoa yao, walipata mafunzo ya vitendo juu ya matumizi ya Smart DAS na jinsi inavyoweza kuunganishwa na mifumo mingine ya usimamizi wa kodi.
Wakati wa mafunzo hayo, maafisa walishiriki pia katika warsha ambapo walikubaliana juu ya hatua muhimu za kuchukua, ikiwemo kuanzishwa kwa mfumo wa mafunzo kwa ngazi ya chini. Kila afisa sasa anatarajiwa kuendesha warsha za walipa kodi katika ngazi ya mkoa ili kuhakikisha kuwa wazalishaji wote wanaifahamu na kuitumia programu hii mpya bila kuathiri shughuli zao.
“Ufanisi wa Smart DAS unategemea uelewa na upatikanaji wa taarifa,” aliongeza Bw. Tweve. “Maafisa wetu sasa wana ujuzi wa kutosha kuwaongoza walipa kodi, kujibu maswali yao, na kuhakikisha kila mtumiaji anaelewa faida za kutumia teknolojia ya kidijitali.”
Kama sehemu ya mpango huu, SICPA Tanzania imetoa kadi za uhakiki (validator cards) 5,000 za ziada kwa TRA. Kadi hizi, ambazo zina madirisha mawili yanayoonesha athari ya rangi za usalama kwenye stempu halali, zitasambazwa kwa wauzaji wa jumla, wasambazaji, na wadau wengine katika mnyororo wa usambazaji wa bidhaa za ushuru wa bidhaa, ili kuimarisha ushirikishwaji wa wadau. Kadi hizi hurahisisha uhakiki wa stempu kabla ya bidhaa kukubaliwa.
“SICPA Tanzania inajivunia kushirikiana na TRA katika kusambaza zana salama na za kisasa za kulinda mapato ya serikali na kukuza biashara yenye usawa,” alisema Alfred Mapunda, Meneja Mkuu wa SICPA Tanzania. “Kadi za uhakiki na suluhisho la Smart DAS ni sehemu ya dhamira yetu ya kuisaidia Tanzania katika safari yake ya kuelekea kwenye usimamizi wa kodi ulio wazi, wa kisasa na wa kuaminika.”
Kwa kuchanganya teknolojia na mafunzo, ushirikiano huu ni hatua kubwa kuelekea katika juhudi za serikali kulinda mfumo wa ushuru wa bidhaa na mapato yanayotokana nao. Mpango huu hauishii tu katika kuziba mianya ya uzingatiaji bali pia unawapa wajasiriamali na wafanyabiashara zana rafiki zinazowahamasisha kuzingatia kodi kwa hiari.
Katika kipindi ambacho mabadiliko ya kidijitali yanachukua nafasi kubwa katika taasisi za ukusanyaji mapato barani Afrika,Tanzania inaonesha uongozi wa kikanda kupitia ubunifu wa vitendo unaojibu mahitaji ya serikali na sekta binafsi, pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Kenya na Uganda.