SERIKALI imetenga kiasi cha Shilingi milioni 200 kwa ajili ya Motisha kwa watoa taarifa za ukwepaji Kodi na wabunifu watakaoweza kubuni namna bora ya kukusanya Kodi na kuongeza wigo wa ukusanyaji Kodi kwa Maendeleo ya Nchi.
Hayo yamesemwa leo Aprili 8, 2025 na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda kwenye Kongamano la kwanza la Kodi lililiofanyika jijni Dar es Salaam likiwa na Kauli mbiu ya “kuongeza wigo wa kodi na kuimarisha ulipaji wa kodi kwa hiari’. ambalo lilienda sambamba na uzinduzi wa motisha mbili; ya mtoa Taarifa za kikodi na mawazo bunifu ya kukusanya Kodi.
“Leo tumezindua mambo mawili ya kuweza kutoa Motisha kwa wale Vijana na watu wengine wenye mawazo ya namna gani tukusanye kodi kwa amani huku watu wakifurahia watuletee…..tumetenga Sh. Milioni 200 za kutoa mkitupa hayo mawazo yakiwa bora kuliko mengine,” amesema Mwenda.
Ameongeza kuwa eneo lingine la Motisha watakalotoa ni kwa wale watakaofichua wakwepa Kodi ambapo itatolewa kuanzia sh.milioni moja hadi milioni 20 kulingana na kiasi kitakachokusanywa endapo watabaini ukweli.
Aidha Mwenda amewataka wafanyabishara wa mitandaoni na wahamasishaji (Influencers) kujiandika ili waweze kulipa kodi kwa hiari.
“Kwa mujibu wa Sheria zetu Biashara za mitandaoni na influencer hazijasamehewa kodi, hivyo wanapaswa kulipa Kodi na wengine tayari wameshafikiwa kuelimishwa na kuweza kulipa kodi ya Serikali.
Amesema sheria inamtaka kila Mtu anayefanya Biashara zaidi ya Sh. Milioni nne kwa Mwaka alipe Kodi.
“Wasipofanya hivyo wakifuatwa na kutambuliwa na watu wetu watahesabiwa tangu walipoanza biashara na kuanza kulipa Riba na faini, “niwasihi wajitokeze waelimishwe ili wasifikie huko” amesisitiza Mwenda.
Awali akifungua Kongamano hilo, Naibu Waziri ofisi ya Rais mipango na uwekezaji, Stanslaus Nyongo ameitaka TRA kufanyia kazi mawazo yote yatakayotolewa na wadau ili kuweza kufikia malengo kusudiwa.
“Imekuwa ni kawadia mijadala inafanyika lakini haifanyiwi kazi, niwatake muhakikishe maoni yote yanayotolewa na hawa wadau , watafiti, wafanybaishara na walipa Kodi yakusanywe pamoja na kuweza kuyafanyia kazi,” amesema Nyongo.
Amesema kabla ya kufanyika kwa Kongomano lingine maoni yote yaliyotolewa Leo ni vema yakafanyiwa tathmini na kuona kama wameweza kufikia malengo ya kuongeza wigo wa walipa Kodi.
Hata hivyo, Nyongo amesema urasimilisjai wa Biashara nchini uko chini hivyo TRA wana jukumu kubwa la kutoa elimu.
Pia amewataka watumie jukwaa hilo kuweza kutoka hapo walipo watoke na mbinu mpya ya kuongeza wigo wa kodi na namna ya kuweza kurasimimisha biashara zisizo rasmi.
Waziri amependekeza pia kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kuhamasisha malipo ya digitali akitolea mfano wa vituo vya mafuta vyote zikiweka mfumo kuwa kila anayekwenda kujaza mafuta alipe kwa digital.
Kwa upande wake,Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA), Profesa Isaya Jairo amesema kongamano hilo limekusudia kujadili changamoto na kutoa majibu ya pamoja kwa suala la ulipaji kodi nchini.
“Tunahitaji kujua kwa nini baadhi ya watu hawalipi kodi au hawalipi kodi sahihi. Kupitia majadiliano haya tutapanua uelewa na kushirikiana kusaidia serikali kupata kodi stahiki,” amesema Profesa Jairo.
Kongamano hilo linafanyika kwa mara ya kwanza na linatarajiwa kuwa jukwaa la kudumu la mijadala kuhusu masuala ya kodi, likilenga kuimarisha uhusiano kati ya walipa kodi na mamlaka za serikali.