…………..
Na Mwandishi wetu.
Jitihada kubwa za kukuza Utalii nchini zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, zinazidi kushamiri katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa Gofu nje kidogo ya Hifadhi hiyo ilioko Mkoani Mara.
Akikagua ujenzi wa uwanja huo wenye mvuto wa kipekee, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema ujenzi wa uwanja huo ni jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendelea kukuza sekta ya Utalii ili kuongeza zaidi furasa kwa watanzania kupitia watalii wanaoingia nchini pamoja na kukuza pato la Taifa.
Aidha Dkt. Abbasi ameridhishwa na kasi ya ujenzi unaendelea ambao umefikia hatua nzuri na pindi utakapo kamilika utaongeza mchechemko wa watalii nchini hususani wa michezo.
Dkt. Abbasi licha ya kupongeza kwa kazi nzuri ya usimamizi wa unjenzi huo, amesisitiza kasi zaidi ili ukamilike kwa wakati uliopangwa na kutoa nafasi ya kuendelezwa kwa viwanja vingine kadha vya michezo ambayo yatakuwa ni mazao mapya ya Utalii wa Michezo.
Uwanja huo unaojengwa nje kidogo ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama sehemu ya kuibua zao jipya la utalii wa michezo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwaka huu.