Dar es Salaam, Mei , 2025 — Benki ya Absa Tanzania
imethibitisha kwa mara nyingine nafasi yake kama mshirika mkuu katika maendeleo
ya uongozi wa kifedha katika ukanda wa Afrika Mashariki, baada ya kudhamini kwa
mafanikio Mkutano wa 10 wa Maafisa Wakuu wa Fedha (CFO), uliofanyika jijini Dar
es Salaam.
Mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Serena uliwaleta
pamoja zaidi ya wataalamu 100 waandamizi wa masuala ya fedha (CFOs) kutoka nchi
mbalimbali za Afrika Mashariki, ambapo walibadilishana uzoefu, kujadili
mitazamo mipya na kuimarisha mahusiano ya kitaaluma katika sekta ya fedha.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser, alisema udhamini wa benki ya ABSA unaendana na
dhamira ya kuendeleza Afrika kwa kusaidia taasisi na viongozi wake wa kifedha
(CFOs).
“ABSA Bank Tanzania tukiwa kama wadhamini wakuu wa mkutano
huu, tunatambua nafasi nyeti ya viongozi wa fedha (CFOs) katika kusuka
mustakabali wa taasisi mbalimbali barani Afrika Mashariki; Nafasi ya CFO
imepanuka zaidi ya usimamizi wa kifedha wa jadi; sasa inahusisha ubunifu,
mageuzi ya kimkakati na uundaji wa thamani ya muda mrefu.” Alisema Bw. Obedi
Laiser.
Alibainisha kuwa benki hiyo inaendelea kutoa suluhisho
mahususi ya kifedha na ushauri wa kimkakati ili kusaidia taasisi mbalimbali
kustawi katika mazingira ya kiuchumi yenye changamoto nyingi.
“Tupo tayari kushirikiana na maafisa wa fedha kwa kuwapatia
maarifa, mitaji na utaalamu utakaowasaidia kufanikisha malengo yao na kufungua
fursa mpya za ukuaji,” aliongeza Bw. Laiser.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika mkutano huo ni
pamoja na mabadiliko ya nafasi ya CFO, mageuzi ya kidijitali, ujumuishaji wa
masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG), pamoja na mbinu bora za
ukuaji wa kimkakati na usimamizi wa mitaji.
Kwa mujibu wa waandaaji, mkutano huo ulikuwa jukwaa muhimu
kwa wataalamu wa fedha kuandaa mbinu za kukabiliana na changamoto zinazoikumba
sekta hiyo, sambamba na kuimarisha mwelekeo wa ukuaji endelevu wa biashara
katika ukanda huu wa Afrika.
Ushiriki wa Absa Tanzania unaenda sambamba na kauli mbiu
yake ya “Stori yako ina thamani” kuwawezesha waafrika kupitia ushirikiano wa
kimkakati, ubunifu na uongozi wa fikra. Ikiwa na mtandao mpana na
uliojiimarisha unaovuka nchi zaidi ya 10 barani Afrika pamoja na ofisi zake
London, New York, Namibia na Nigeria, Absa inaendelea kuwa muhimili muhimu
katika kukuza uchumi na ujumuishaji wa kifedha.
Mkutano huo ulifungwa kwa wito kwa viongozi wa fedha Afrika
Mashariki kuendelea kujifunza, kushirikiana na kuwa wabunifu ili kujenga
uthabiti katika mazingira ya kifedha yanayobadilika kwa kasi.