Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam, 16 Mei 2025 – Taasisi ya UONGOZI inatarajia kuendesha sherehe ya mahafali yake ya nane leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi 200 kutoka sekta mbalimbali wanatarajiwa kutunukiwa vyeti baada ya kukamilisha programu za muda mrefu za mafunzo ya uongozi.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Boniface Simbachawene (Mb).
Wasilisho kuu katika tukio hilo litatolewa na Bibi Suzanne Innes-Stubb, Mke wa Rais wa Finland, ambaye pia ni mtaalamu mwandamizi wa kimataifa katika masuala ya sheria na maadili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Taasisi hiyo, Bi Suzana Aroko, wahitimu wa mwaka huu wamepata mafunzo kupitia programu tatu kuu ambazo ni:
Stashahada ya Uzamili ya Uongozi (Postgraduate Diploma in Leadership)
Programu ya Uongozi Ngazi ya Cheti (Certificate in Leadership)
Programu ya Uongozi kwa Wanawake (Women’s Leadership Programme.
Sherehe hiyo pia inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, wakiwemo wawakilishi kutoka sekta ya umma, binafsi, elimu ya juu pamoja na asasi za kiraia.
Programu hizi zinalenga kukuza uwezo wa viongozi katika maeneo ya sifa binafsi za uongozi, usimamizi wa rasilimali watu, na uongozi wa taasisi, kwa namna inayowawezesha kuendelea kujifunza bila kuathiri majukumu yao ya kila siku.
Stashahada ya Uzamili ya Uongozi pamoja na Programu ya Uongozi Ngazi ya Cheti zinatekelezwa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Aalto cha Mafunzo ya Utawala, kilichopo nchini Finland, huku Serikali ya Tanzania na Finland zikiwa wadhamini wakuu.
Kwa upande mwingine, Programu ya Uongozi kwa Wanawake inafadhiliwa kwa pamoja na Serikali hizo mbili, Umoja wa Ulaya (EU), na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women).
Taasisi ya UONGOZI imesisitiza kuwa ushiriki katika tukio hilo ni kwa mwaliko maalum pekee