Mwamvua Mwinyi,Mafia
Mei 17,2025
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Mafia, Omar Kipanga, ametoa rai kwa wadau wa elimu wakiwemo viongozi, walimu na wazazi kushirikiana na Serikali kuihamasisha jamii kuwawezesha watoto wa kike kuvuka vizingiti vya kimfumo na kijamii vinavyowazuia kupenda na kufanya vizuri katika masomo ya sayansi.
Akizungumza Mei 17, 2025, wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuhamasisha wanafunzi wa kike kupenda masomo ya STEM, unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya UNESCO (NatCom) kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Kipanga alisema, mradi huo umekuja kwa wakati muafaka.
“Tunatambua jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuweka mazingira bora ya mtoto wa kike kupata elimu,
“Ni wajibu wetu sasa kuwahamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi kama ilivyo masomo mengine ili wasiachwe nyuma katika mapinduzi ya sayansi na teknolojia.”
Dkt. Joel Samuel, Mkuu wa Kitengo cha Sayansi Asilia kutoka Tume ya Taifa ya UNESCO, akimwakilisha Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, alieleza kupitia mradi huo, Tume itashughulikia changamoto ya uhaba wa walimu wa sayansi kwa lengo la kuhakikisha mradi unakuwa endelevu na kuleta matokeo chanya .
Mwajuma Ibrahim mjumbe wa bodi ya shule ya sekondari Kitomondo alisema, akiwa kama mzazi na mlezi atakuwa balozi kwa kutembelea kila shule katika kata ya Kiegeani kuwahamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi.
“Takwimu zinaonyesha kuwa, ingawa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mchepuo wa sayansi imeongezeka kutoka 21 mwaka 2020 hadi 55 mwaka 2023, bado uwiano kati ya wasichana na wavulana haujaridhisha, huku wavulana wakiongoza kwa idadi na ufaulu.”
Khadija Mohamed, mwalimu wa Baiolojia kutoka shule ya sekondari Kitomondo, alifafanua kuwa ,bado kunahitajika juhudi kubwa kuhakikisha watoto wa kike hawakatishwi tamaa.
“Walimu tunapaswa kuwa marafiki wa watoto wa kike na kuwawezesha kupenda masomo ya sayansi, Mwaka 2024, mwanafunzi wa kike alipata alama ya ‘A’ katika Baiolojia, jambo linaloonesha kuwa tunaweza tukiwajali na kuwaongoza ipasavyo.”
Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuchukua hatua katika kuboresha elimu ya mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule maalum 26 za wasichana za sayansi, mabweni na utekelezaji wa programu mahsusi kama Samia Scholarship kwa ajili ya kuwasomesha watoto wa kike na kuwaandaa kushiriki katika maendeleo ya Taifa.