


Dakatari Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Fionna Mercy (wa kwanza kulia) akitumia kifaa tiba (Defibrillator Mashine) kumpima moyo Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, wakati wa uzinduzi kambi ya siku mbili ya uchunguzi wa afya ya moyo iliyofanyika leo Mei 21, 2025, Dar es Salaam katika Kampasi ya Mloganzila, Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, ikiwa na lengo la kusaidia wananchi kuboresha afya zao pamoja na kutoa elimu ya afya jambo litachangia maendeleo ya Taifa (PICHA NA NOEL RUKANUGA)





Wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wakipata huduma ya uchunguzi wa afya ya moyo katika Kampasi ya Mloganzila, Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu


Mteknolojia wa Maabara kutoka MUHAS Bw. Joseph Temba (wa kwanza kulia) akitoa ufafanuzi kwa Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa namna kitengo za mazoezi kinavyofanyakazi.
…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeweka kambi ya siku mbili ya uchunguzi wa afya ya moyo katika Kampasi ya Mloganzila, Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, ikiwa na lengo la kusaidia wananchi kuboresha afya zao pamoja na kutoa elimu ya afya jambo linachangia maendeleo ya Taifa.
Kambi hiyo, inayotoa huduma bure, imeanza rasmi leo Mei 21 hadi Mei 22, 2025 ambapo Wananchi wanapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo, kujifunza kuhusu visababishi vya magonjwa hayo, matumizi sahihi ya dawa, kupata huduma saidizi pamoja na kutembelea mabanda ya maonesho ya bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na wataalamu wa MUHAS, hasa kutoka sekta ya Famasia na Dawa za Tiba Asilia.
Akizungumza leo Mei 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa amesema kuwa kambi hiyo imelenga kusaidia Taifa kutokana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa, hasa yale yanayotokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha, ikiwemo aina ya vyakula vinavyotumika.
Prof. Kamuhabwa amesisitiza umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini uwepo wa tatizo la moyo mapema pamoja na kupewa ushauri kuhusu namna ya kuzuia au kutibu magonjwa hayo.
“MUHAS tunatoa shahada ya kwanza na ubobezi kwenye masuala ya afya ya moyo. Tuna wataalamu wa kutosha, tunafanya tafiti na kutoa huduma za afya kwa jamii,” amesema Prof. Kamuhabwa.
Ameongeza kuwa, kupitia vifaa Tiba vya kisasa vya uchunguzi vilivyopo, wananchi watakaobainika kuwa na matatizo ya afya ya moyo wataelekezwa katika vituo husika kwa ajili ya matibabu zaidi.
Katika hatua nyingine, Prof. Kamuhabwa ameeleza kuwa kambi hiyo ni sehemu ya maandalizi kuelekea uzinduzi wa awamu ya pili ya Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotarajiwa kufanyika Mei 23, 2025.
“Awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa jengo la mafunzo lenye kituo cha mazoezi, maabara, na kumbi za mikutano. Awamu ya pili itajumuisha ujenzi wa hospitali ya magonjwa ya moyo, ufundishaji, programu za kufikia jamii, pamoja na utoaji wa huduma za afya,” amesema Prof. Kamuhabwa.
Amebainisha kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo atakuwa Waziri wa Elimu, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, akiambatana na viongozi mbalimbali wa serikali, mashirika binafsi pamoja na wananchi.
Katika uzinduzi huo, kutakuwa na matukio mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa magari mawili ya kubebea wagonjwa pamoja na maabara maalumu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma MUHAS , Prof. Emmanuel Balandya, amesema kuwa MUHAS kwa sasa inatoa jumla ya programu 93 za ubobezi zenye lengo la kuendelea kuzalisha wataalamu katika fani mbalimbali, ikiwemo magonjwa ya ndani, magonjwa ya watoto, na moyo.
Nao wananchi waliotembelea kambi hiyo, akiwemo Bi. Maria Tadei na Bw. Emmanuel John, wameishukuru MUHAS kwa kutoa huduma bora za vipimo vya moyo, huku wakieleza kuwa zimewasaidia kufahamu hali ya afya zao na kupata mwelekeo sahihi wa matibabu.