Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila kinatarajia kuanzisha kozi ya muda mfupi itakayofundisha namna bora ya kuwaongoza watu kufanya mazoezi ya mwili (GYM) bila kupata madhara ya kiafya.
Hatua hii inalenga kukabiliana na changamoto inayosababishwa na baadhi ya vituo vya mazoezi nchini vinavyoendesha mazoezi bila kuzingatia afya za wahusika, wakiwemo watu wenye matatizo ya kiafya yanayohitaji mazoezi maalum.
Akizungumza leo Mei 21, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kambi ya uchunguzi wa afya ya moyo iliyofanyika kwa siku mbili kuanzia Mei 21 – 22, 2025 katika Kampasi hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema kuwa kozi hiyo inalenga kuhamasisha jamii kupima afya kabla ya kuanza mazoezi yoyote.
“Ni muhimu mtu kupima afya kabla ya kuanza mazoezi. Mazoezi ni muhimu, lakini yanapofanyika bila uelewa sahihi yanaweza kusababisha madhara makubwa kiafya,” amesema Prof. Kamuhabwa.
Akizungumzia Kambi hiyo ya afya, ameeleza kuwa ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa awamu ya pili ya Kituo cha Umahiri cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Huduma za Moyo, ikiwa ni mkakati wa MUHAS kukabiliana na ongezeko la magonjwa ya moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Uchunguzi wa mapema unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za matibabu na kuokoa maisha ya watu. Kambi hii imekuja wakati ambapo takwimu za magonjwa ya moyo zinaongezeka kwa kasi,” aliongeza Prof. Kamuhabwa.
Kwa sasa, MUHAS inatoa jumla ya programu maalumu 93 za kitaaluma, zikiwemo Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Tiba, programu za Tiba ya Moyo kwa Watoto, na Misingi ya Moyo—ambazo kila moja hupokea wanafunzi 10 hadi 20 kwa mwaka.
Aidha, MUHAS imejipanga kupanua mitaala yake kwa kuanzisha programu mpya katika nyanja ya upasuaji wa moyo na uuguzi, ili kuongeza wigo wa wataalamu wanaohitajika kukidhi mahitaji ya huduma za afya nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.