Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Tanga
Usalama wa maisha ya binadamu ni jambo la msingi sana, na ndiyo maana unapaswa kulindwa kwa gharama zote. Katika suala la usalama barabani ambalo ni muhimu katika kuhakikisha raia wanakuwa salama dhidi ya ajali na majanga mengine yanayoweza kutokea barabarani, suala la madereva wenye sifa stahiki kwa maana ya kuhudhuria mafunzo ya udereva katika vyuo mbalimbali linasisitizwa sana.
Kimsingi, ni kosa kisheria kwa dereva wa pikipiki au gari kuendesha chombo cha moto barabarani bila kuwa na leseni ya udereva. Hii inasisitiza watu kuhudhuria kwanza mafunzo ya udereva, kuhitimu na kupata leseni, ndipo waingie barabarani kuendesha vyombo vya moto. Lakini sheria hii inakiukwa na baadhi ya madereva kukosa leseni zinazotambulika. Wanachofanya baadhi yao ni kujifunza kuendesha vyombo vya moto mitaani na kuingia barabarani, jambo linaloongeza ajali na kusababisha ulemavu na vifo kwa watumiaji wa barabara.
Madereva waliopo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Wamiliki na Waendesha Pikipiki na Bajaji Tanga (UWAPIBATA) wanakabiliwa na tatizo la kuendesha vyombo vya moto kama pikipiki maarufu bodaboda na bajaji wakiwa hawana leseni za udereva, jambo linalowaathiri sana kwa kuhatarisha maisha yao na kupigwa faini na askari wa barabarani (trafiki). Kutokana na hali hiyo, wakaamua kuanzisha mfuko wa kukopeshana fedha ili waweze kurasimisha kazi yao kwa kuhudhuria mafunzo kikamilifu ili wapate leseni za udereva.
Kutokana na mahitaji makubwa ya fedha waliyonayo kumudu kulipia mafunzo ili wapate leseni wakawasilisha ombi la fedha kwa Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini (CCM), Ummy Mwalimu, ili aweze kuwasaidia fedha za kutunisha mfuko wao huo ili kuwezesha madereva wengi zaidi kupata mafunzo na hivyo kupata leseni na hatimaye kuwa salama barabarani na kuongeza vipato vyao kupitia kazi yao ya udereva wa pikipiki na bajaji.
Januari 04, 2025, katika viwanja vya Lamore jijini Tanga, Mbunge Ummy Mwalimu alikabidhi fedha kiasi cha Shilingi 10,000,000 (Milioni Kumi) kwa viongozi wa UWAPIBATA ili ziweze kuwasaidia katika kupata mafunzo vyuoni ili kuongeza kasi ya madereva wenye leseni Tanga Mjini . Katika hafla ya kukabidhi fedha hizo, Ummy Mwalimu alisema ” Bodaboda ni kazi kama kazi nyingine, mimi kama Mbunge wa Tanga Mjini nitaendelea kuwathamini na kushirikiana nao ili kuboresha mazingira ya kazi zao”.
Kitendo cha kuwaunga mkono madereva bodaboda na bajaji ni miongoni mwa mkakati wa Ummy Mwalimu kuwawezesha wananchi kiuchumi hasa vijana kwa kuzingatia kuwa kundi hili ni kubwa, na mafanikio yao kiuchumi yanawezesha pia ustawi wa familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
Ni jambo la faraja kuona, fedha hizo zimeleta athari chanya kwani baadhi ya madereva wa bodaboda na bajaji wamepata mafunzo ya udereva na kupata leseni zao, hivyo kufanya shughuli zao za udereva kwa uhuru lakini pia kuongeza vipato vyao na kuongeza usalama wa maisha yao kwani sasa ni madereva mahiri wanaojua sheria, miongozo na kanuni za usalama barabani.
Kwa hakika, madereva bodaboda na bajaji Tanga Mjini wamepata tabasamu kupitia Shilingi Milioni Kumi zilizotolewa na Mbunge wao Ummy Mwalimu, na hivyo kupata leseni za udereva, jambo ambalo lilikuwa kilio chao cha muda mrefu, lakini sasa limepatiwa ufumbuzi.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800 462.