Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (katikati) akibonyeza kitufe ikiwa ni ishara ya uzinduzi mradi wa awamu ya pili wa ujenzi na uendelezaji wa Kituo cha Umahiri wa Sayansi ya Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) katika hafla iliyofanyika leo, Mei 23, 2025, jijini Dar es Salaam katika Kampasi ya Mloganzila (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (katikati) akikata utape ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa magari ya kubebea wagonjwa ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) katika hafla iliyofanyika leo, Mei 23, 2025, jijini Dar es Salaam katika Kampasi ya Mloganzila.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (katikati) akikata utape ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo kwa Vitendo, Tiba za dharura na Ajali katika Kampasi ya Mloganzila.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari wakati akizindua mradi wa awamu ya pili wa ujenzi na uendelezaji wa Kituo cha Umahiri wa Sayansi ya Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa awamu ya pili wa ujenzi na uendelezaji wa Kituo cha Umahiri wa Sayansi ya Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha MUHAS, Bi. Marsha Macatta Yambi akizungumza na waandishi wa habari wakati uzinduzi wa mradi wa awamu ya pili wa ujenzi na uendelezaji wa Kituo cha Umahiri wa Sayansi ya Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotekelezwa na MUHAS.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dkt. Felix Bundala akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa awamu ya pili wa ujenzi na uendelezaji wa Kituo cha Umahiri wa Sayansi ya Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amezindua mradi wa awamu ya pili wa ujenzi na uendelezaji wa Kituo cha Umahiri wa Sayansi ya Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Mradi huo unatekelezwa katika Kampasi ya Mloganzila ya MUHAS, ukigharimu dola milioni 83 kupitia mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), na unasimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. kupitia mradi huu, hospitali ya kisasa ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu itajengwa pamoja na kuwekwa vifaa tiba vya kisasa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyokwenda pamoja na uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo kwa Vitendo, Tiba za Dharura, magari ya kubeba wagonjwa, iliyofanyika leo, Mei 23, 2025, jijini Dar es Salaam katika Kampasi ya Mloganzila, Profesa Mkenda, amesema kuwa kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kutoa tiba ya hali ya juu kwa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
Profesa Mkenda ameongeza kuwa hospitali itakayojengwa itakuwa tofauti na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, huku akifafanua kuwa kutakuwa na vituo maalumu kwa ajili ya upasuaji na matibabu ya moyo na mishipa ya damu.
“MUHAS inafanya kazi nzuri, ikiwemo utafiti na ugunduzi wa dawa mbalimbali kwa ajili ya kusaidia jamii, kama vile zile za kutibu tezi dume na shinikizo la damu. Tunatarajia kuongeza bajeti ili tafiti hizi zikamilike na kuwa msaada kwa wananchi,” amesema Profesa Mkenda.
Ameeleza kuwa MUHAS ni chuo bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kufanya tafiti za kitabibu, hivyo serikali itaendelea kushirikiana na chuo hicho ili kufanikisha mafanikio makubwa zaidi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema kuwa kuwepo kwa kituo hicho kutachangia maendeleo ya miradi mbalimbali ya chuo, huku akitoa shukrani kwa wafanyakazi na wanafunzi wa MUHAS kwa ushirikiano wao.
Profesa Kamuhabwa amesema kuwa chuo kitaendelea kufanya tafiti na kuwashirikisha watunga sera pamoja na wadau mbalimbali ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.
“Tutahakikisha tafiti tunazozifanya zinajulikana, pamoja na kuandaa miongozo na mapendekezo kwa watunga sera ili kuboresha huduma za afya nchini,” amesema Profesa Kamuhabwa.
Ameeleza pia kuwa mwaka huu, chuo kimeandaa Kongamano la 15 la Kisayansi lenye kaulimbiu: Kurekebisha Mifumo ya Afya Barani Afrika: Kipaumbele kwa Watumishi na Utafiti ili Kukabiliana na Changamoto za Afya za Dunia Zinazoendelea.
Kongamano hilo litafanyika Juni 18 – 19, 2025, katika Kituo cha Umahiri wa Sayansi ya Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, Mloganzila, Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dkt. Felix Bundala, amepongeza MUHAS kwa kutoa huduma bora kwa wanafunzi na kwa mchango wake katika utafiti na utoaji wa huduma katika sekta ya afya.
Amesema utekelezaji wa majukumu ya MUHAS unakwenda sambamba na sera ya Wizara ya Afya, ikiwemo kuzindua programu ya huduma kwa watoto wachanga.
Ameongeza kuwa takwimu zinaonesha kuwa watoto milioni 2.4 huzaliwa kila mwaka duniani, huku 50,000 wakifariki kutokana na matatizo ya kiafya.
“Tumeshuhudia kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchi yetu ikipokea tuzo kwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Juhudi za MUHAS katika kutekeleza miradi hii ni sehemu ya mkakati wa kupunguza vifo vya watoto wachanga,” amesema Dkt. Bundala.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha MUHAS, Bi. Marsha Macatta Yambi, amesema kuwa kituo hicho kitasaidia jamii kwa kuhamasisha umuhimu wa kutambua hali ya afya ya moyo na mishipa ya damu, ili waweze kuchukua hatua mapema na kupata matibabu sahihi.