Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akizindua mradi wa Maji Malamba utakaowanufaisha Wananchi zaidi ya 2,463 wa Vijiji vya Malamba na Mkuranga Halmashauri ya Mji Nanyamba Mkoa wa Mtwara,kulia Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdala Mwaipaya.
Baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha Malamba Halmashauri ya Mji Nanyamba Mkoani Mtwara,wakisubiri kupokea Mwenge wa Uhuru katika Kijiji hicho kwa ajili ya kuzindua mradi wa Maji.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akiangalia mchoro wa mradi wa maji Malamba Halmashauri ya Nanyamba Mkoa wa Mtwara kabla ya kutembelea na kuzindua mradi huo utakaowanufaisha zaidi ya Wananchi 2,463 wa Kijiji cha Malamba na Mkuranga,kushoto Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdala Mwaipaya na kulia aliyeshika fimbo Meneja wa Ruwasa Hamis Mashindike.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akifungua koki baada ya kuzindua mradi wa Maji Malamba Halmashauri ya Mji Nanyamba Mkoani Mtwara uliotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa)Wilaya ya Mtwara ambao utahudumia zaidi ya Wananchi 2,463 wa Vijiji vya Malamba na Mkuranga,ushoto Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdala Mwaipaya.
Muonekano wa vituo vya kuchotea maji vilivyojengwa kupitia Mradi wa Maji Malamba ambavyo vitanatoa huduma ya maji kwa Wananchi wa Kijiji cha Malamba.
Nyumba ya mashine(Pump House)
……….
Na Mwandishi Maalum, Mtwara
TAKRIBANI Wakazi 2,463 wa kijiji cha Malamba na Mkulanga Halmashauri ya Mji Nanyamba Mkoani Mtwara, wameondokana na kero ya majisafi na salama baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA) kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji Malamba uliogharimu Sh. 94,330,350.49 kati ya Sh.101,079,008.5 zilizotengwa kutekeleza mradi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdala Mwaipaya alisema,awali wananchi wa vijiji hivyo hawakuwa na huduma ya maji ya uhakika kwa kuwa kisima kilichokuwepo kuzalisha kiasi kidogo cha maji.
Alisema,kutokana na changamoto hiyo Serikali imeamua kuboresha kisima hicho ili wananchi waweze kupata huduma ya maji ya uhakika na kumaliza mateso ya kukaa kwa muda mrefu kwenye vyanzo vingine vya asili kusubiri kupata maji.
Mwaipaya,amemshukuru Rais kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Mtwara ambayo imewezesha wananchi wa vijiji mbalimbali kupata huduma za kijamii kwa urahisi kwenye maeneo yao.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike alisema,mradi wa Maji Malamba ulianza kutekelezwa Mwezi Januri na kukamilika Mwezi Mei mwaka huu chini ya usimamizi wa Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)Wilaya ya Mtwara.
Alisema,fedha za mradi huo zimetoka Wizara ya maji chini ya Mfuko wa Taifa wa Maji na unatekelezwa kwa kutumia wataalamu wa ndani kikundi cha Juhudi-Masasi na utekelezaji wake umefikia asilimia 100.
Alisema,mradi huo unahudumia zaidi ya wananchi 2,463 kati yao 1,290 wanatoka Kijiji cha Malamba na 1,173 Kijiji cha Mkuranga na hadi sasa fedha zilizolipwa ni Sh.94,330,350.49.
Mashindike alisema, mradi wa Maji Malamba umeanzishwa ili kusogeza na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba.
“Katika utekelezaji wa mradi huu kazi zilizofanyika ni kuchimba kisima kirefu kimoja,kusambaza maji,kufunga pampu,kufunga nishati ya umeme jua,kukarabati tenki la ujazo wa lita 25,000 juu ya mnara wa mita 3 katika Kijiji cha Mkuranga,kukarabati nyumba ya mitambo na kujenga vituo 3 vya kuchotea maji”alisema Mashindike.
Alisema,utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 100 na utakabidhiwa kwa chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya Jamii(CBWSO) kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi.
Fundi aliyejenga mradi huo Alfred Mwambene,ameishukuru Serikali kwa kuwaamini mafundi wadogo na wazawa kwenye kutekeleza miradi ya maji,hata hivyo ameiomba Serikali kuwapa kazi ili kuwajengea uwezo na uzoefu utakaosaidia Nchi yetu kupata mafundi na wakandarasi wazawa wenye uchungu nan chi yao badala ya kutumia wataalamu wa nje.
Kwa upande wake,Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,amewaomba wananchi kushirikiana na Serikali katika kutunza na kulinda miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji inayotekelezwa kwenye maeneo yao.
Alisema,Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha mapenzi makubwa kwa wananchi baada ya kutoa fedha zaidi ya Sh.milioni 101 ili kuboresha huduma ya majisafi na salama katika vijiji hivyo,kwa hiyo haitakuwa na maana iwapo mradi huo hautadumu kwa muda mrefu na kushindwa kuleta tija iliyokusudiwa.
Baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha Malamba wameipongeza Serikali kukamilisha ujenzi wa mradi huo ambao umesaidia kumaliza kero ya kuamka usiku wa manane kwenda vijiji vya jirani kutafuta maji kwa matumizi yao.
Wamesema, kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida ya kutembea umbali mrefu hali iliyopelekea kushindwa kufanya shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo kilimo na biashara ndogo ndogo.
Ali Mfaume alisema,kabla ya mradi huo walikuwa wanatembea kati ya kilometa 2 hadi tatu kwenda vijiji vya jirani kutafuta maji yanayopatikana kwenye mito na mabonde ambayo hayakuwa afi na salama kwa matumizi ya Binadamu.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Said Abdala alisema, awali walilazimika kwenda mbali kufuata maji kwa matumizi yao ya kila siku jambo lililorudisha nyuma maendeleo yao kwa kuwa walipoteza muda mwingi kwenda kutafuta maji badala ya kushiriki katika kazi za maendeleo.
Ameipongeza Wizara ya Maji kupitia Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)Wilaya ya Mtwara kukamilisha ujenzi wa mradi uliomaliza kero na mateso ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda wao mwingi kwenda kutafuta maji.