Maswa, Mei 20, 2025
Mahakama ya Wilaya ya Maswa imemhukumu Bw. Masanja Andrew Mboje (36), Katibu wa Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) cha Gula, kifungo cha miaka 20 jela pamoja na agizo la kurejesha kiasi cha Shilingi 3,518,000/= alizozifanyia ubadhirifu.
Taarifa iliyotolewa na TAKUKURU wilaya ya Maswa imesema Bw. Mboje alifikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa ya ubadhirifu na ufujaji wa mali ya umma, kinyume na Kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [Sura ya 329, Marejeo ya 2022], pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza na Vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa [Sura ya 200, Marejeo ya 2022].
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, mshtakiwa akiwa Katibu wa AMCOS ya Gula na mtu pekee aliyekasimiwa mamlaka ya ununuzi wa pamba kutoka kwa wakulima, alitumia kiasi cha Shilingi 3,518,000/= kwa matumizi binafsi, fedha ambazo zilipaswa kulipwa kwa mkulima Bw. Edward James Mathias.
Kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 196/2025 imesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa, Mheshimiwa Azizi Mzee Khamis (RM), huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Bw. Bahati Madoshi Kulwa.