Na Diana Byera, Bukoba
Shilingi Bilioni 20.6 zimetumika ndani ya kata ya Bakoba, Manispaa ya Bukoba kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi, ikiwemo ukarabati mkubwa wa Bandari ambayo ipo katika kata hiyo.
Diwani wa kata ya Bakoba, Shabani Rashid, amesoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata hiyo na kudai kuwa serikali imetekeleza miradi mikubwa inayogusa jamii ukilinganisha na kipindi kata hiyo ilipokuwa inaongozwa na Diwani wa CHADEMA kwa miaka 15.
Amesema kuwa kuna mabadiliko makubwa sana katika jamii katika miradi ya barabara, afya, maji, na elimu ambayo moja kwa moja imewagusa wananchi mmoja mmoja na kuchochea maendeleo katika kata hiyo.
Anasema kuwa anapoelekea kumaliza miaka mitano ameshuhudia mabadiliko makubwa katika uunganishwaji na ufunguzi wa barabara nyingi katika kata hiyo ambazo hazijawahi kufunguliwa, na sasa wananchi wanayo mawasiliano mazuri ya barabara; ukarabati wa shule ya zamani ambayo ilijengwa kwa tope; ukarabati wa maabara ya kemia; ujenzi wa madarasa; vyoo bora; uwepo wa maji safi na salama ya bomba ukilinganisha na miaka iliyopita.
“Kata hii ilikuwa chini ya upinzani kwa miaka 15. Kama kijana nilipewa dhamana ya kuongoza kata hii, serikali imefanya mambo makubwa sana ambayo hayajawahi kushuhudiwa, hivyo wananchi wanafurahia na imani kati ya wananchi na serikali yao imeongezeka,” anasema Rashid.
Anasema kuwa ameshiriki moja kwa moja katika kushiriki kazi za jamii ikiwemo kugawa bima za afya kwa wananchi wasio na uwezo, kusafisha mazingira ikiwemo mto Kanoni, kujitolea katika ufunguzi wa barabara mpya, kushiriki misiba na sherehe, kununua sare za shule kwa wanafunzi wasio na uwezo, kuandaa ligi za michezo zilizoshirikisha vijana, kuhakikisha mikutano ya hadhara inafanyika inayoonyesha mapato na matumizi.
Alisema maono yake makubwa ni kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa, wananchi kupata huduma nzuri kiafya, miradi ya ujenzi ya kingo za mto Kanoni zinatekelezeka pamoja na kuona jamii ya vijana inayoendelea kukua kwa maadili na kuwa na maono ambayo yanalenga kuleta maendeleo kwa kila mtu.