Katika kuhakikisha huduma za afya zinasogezwa karibu na wananchi kambi ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi maarufu kama “Madaktari wa Samia” imefunguliwa rasmi mkoani Ruvuma kwa awamu ya tatu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kambi ya madaktari bingwa na Ubingwa bobezi Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Mary Makondo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, amesema serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika kusogeza huduma bora za afya kwa wananchi kupitia utaratibu wa kambi hizi.
Kambi ya awamu ya tatu inafanyika kuanzia tarehe 26 Mei hadi 31 Mei 2025, ambapo madaktari bingwa watahudumu kwa siku sita katika hospitali zote za halmashauri ya mkoa wa Ruvuma na Kila hospitali imepangiwa seti ya madaktari bingwa sita pamoja na daktari bingwa mmoja wa fani maalum ikiwa ni pamoja na magonjwa ya wanawake, watoto, mfumo wa mkojo, usingizi na ganzi, afya ya kinywa na meno, na magonjwa ya ndani.
Takwimu zinaonesha kuwa katika awamu ya pili iliyofanyika kati ya tarehe 20 Oktoba hadi 3 Novemba 2024, jumla ya wagonjwa 10,819 walihudumiwa, huku watoa huduma 334 wakipatiwa mafunzo ya kuboresha ujuzi wao ambapo Kambi hiyo ilifanyika katika hospitali sita na vituo vya afya viwili vinavyotoa huduma za upasuaji katika halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma.
Muwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Grace Maliki, Amesema kuwa huduma zitatolewa katika wilaya za Namtumbo, Songea MC, Songea DC, Madaba, Mbinga TC na Nyasa. Akisisitiza kuwa huduma hizo zimeletwa kwa gharama nafuu ili kupunguza adha kwa wananchi wanaohitaji matibabu ya kibingwa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Luis Chomboko, Amesema kuwa ujio wa madaktari hao sio tu kutoa huduma bali pia kuwajengea uwezo wataalamu wa afya waliopo kwenye vituo mbalimbali vya afya ili waendelee kutoa huduma bora hata baada ya kambi kuisha.
Amesema hii ni mara ya tatu kwa madaktari bingwa kuja mkoani humo tangu mwezi Mei 2024.
Dkt. Happiness Komogo, daktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, amesema anatarajia kuwafikia wagonjwa wengi, hasa wale ambao kwa kawaida hushindwa kupata huduma hizo kutokana na changamoto za kiuchumi na kijiografia.
Ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha huduma hizi ni kuwagusa walengwa wa kipato cha chini.
Kwa upande wake Dkt. Bogias Mwamgunda, daktari wa kinywa na meno kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, amesema wamekuja si tu kutoa huduma bali pia kuwajengea uwezo wataalamu wenzao walioko ngazi ya chini ili waweze kuendelea kutoa huduma hizo kwa ufanisi mkubwa.
Katika hitimisho la hotuba yake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma ameishukuru serikali ya awamu ya sita iliyopo chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba vya kisasa, na maboresho makubwa ya miundombinu ya afya jambo ambalo limekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.