Angela Msimbira, Pwani
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Serikali za Mitaa, Bw. Sospeter Mtwale, amefunga rasmi mafunzo ya uongozi kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa, yaliyolenga kuwaongezea maarifa, ujuzi na mbinu bora za kiuongozi kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi katika ngazi za mikoa.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo mkoani Pwani, Bw. Mtwale aliwataka washiriki wa mafunzo kwenda kusimamia kwa weledi na uwajibikaji miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
“Nendeni mkasimamie miradi ya maendeleo kwa kuchukua hatua stahiki pale mnapoona mambo hayaendi sawa. Ufuatiliaji wa miradi ufanyike kwa pamoja na si kwa upande mmoja pekee,” amesisitiza Mtwale.
Ameongeza kuwa ufuatiliaji wa pamoja huimarisha uelewa wa pamoja miongoni mwa watumishi wa umma, na hivyo kuwezesha matumizi bora ya rasilimali chache zilizopo, hatua inayochochea ufanisi wa utekelezaji wa miradi kwa manufaa ya wananchi.
Bw. Mtwale pia amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi kuwa viongozi wa mfano kwa kujenga ushirikiano kazini na kuimarisha timu za kazi zenye mshikamano.
“Kiongozi bora ni yule anayeweza kuwaunganisha watumishi na kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu. Epukeni migogoro inayotokana na maslahi binafsi na gawanyo wa watumishi,” ameongeza.
Amehimiza pia umuhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia maadili ya kazi na kuepuka ubaguzi wa aina yoyote ikiwemo wa kisiasa, kidini au lugha zisizo na staha.
> “Toeni huduma kwa usawa kwa watu wote. Hii ndiyo picha halisi ya Serikali inayowajali wananchi wake,” amesisitiza.
Mafunzo hayo yamewapa washiriki mbinu na nyenzo muhimu kuwa viongozi mahiri, waadilifu na wachapakazi, walioko tayari kutoa huduma bora kwa jamii na kuhakikisha maendeleo ya Taifa yanasimamiwa kikamilifu.