Msajili wa Jumuiya za Kiraia Emmanuel R. M. Kihampa ametoa taarifa ya kufungwa kwa shughuli za kanisa la Glory of Christ Tanzania Church maarufu kama Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima.
Katika taarifa yake Kihampa ameandika; “katika siku za hivi karibuni, kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, umeonekana ukiwa katika mimbari ya
Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church @ Kanisa la Ufufuo na Uzima, ukitoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.
Vitendo hivi ni kinyume cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 chini ya kifungu cha 17 kikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria namba 3 ya mwaka 2019 kwa kuwa vinaathari ya kuhatarisha amani na utulivu nchini.
Hivyo, kwa Mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 17(b) cha Sheria ya Jumuiya sura ya 337 kikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 2019 kilichoifanyia marekebisho kifungu cha 2 cha Sheria ya Jumuiya, nikujulisha kuwa nimefuta usajili wa Glory of Christ Tanzania Church @ Kanisa la Ufufuo na Uzima, kuanzia leo tarehe 02 Juni 2025.
Unatakiwa kusitisha shughuli za Kanisa lako mara moja.” “Kadhalika, unakumbushwa kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 19(1) cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, Jumuiya ya Kiraia iliyofutiwa usajili wake na msajili wa Jumuiya za
Kiraia inayo haki ya kukata rufaa kwa VWaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia kwa Katibu Mkuu kupinga uamuzi huo.
Hivyo, rufaa dhidi ya uamuzi wa kufuta usajili wa Glory of Christ Tanzania Church/ Kanisa la Ufufuo na Uzima inapaswa kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ndani ya siku 21 kuanzia tarehe ya barua hi.”