
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeahirisha kuanza kusikilizwa kwa kesi ya kuchapisha taarifa za uongo inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu kupisha usikilizwaji wa maombi ya Jamuhuri wanaoomba mashahidi wao kufichwa kipindi cha usikilizwaji wa kesi.
Uamuzi huo umetolewa leo Juni 2, 2025 na Hakimu Mwandamizi Geofrey Mhini baada ya kumaliza kusikiliza maombi ya upande wa Jamuhuri ambao waliomba ahirisho la kesi ili maombi yao ya kutaka mashahidi wafichwe wakati wa usikilizwaji yasikilizwe na kutokewa uamuzi.
“Nakubaliana na upande wa mashtaka kwamba kuna sababu za msingi za kuahirish usikilizwaji wa kesi hii kupisha usikilizwaji wa maombi ya Jamuhuri hivyo naiahirisha kesi hii hadi Juni 16, 2025 itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa,”.
Akiwasilisha maombi hayo mapema leo Wakili Wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga amedai uamuzi utakaotolewa katika maombi hayo utawapatia mwangaza wa jinsi gani wataendelea na kesi hiyo.
“Mheshimiwa kesi leo imekuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa lakini tunaleta maombi, tumefaili maombi ya upande mmoja chini ya kifungu cha sheria 188(1) cha kumlinda shahidi na kikiambatana na kifungu 392 (A) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA),”.
Akipinga hoja hizo Wakili wa Utetezi Peter Kibatala amedai upande wa Jamuhuri umeshindwa kutoa taarifa za kutosha kuiwezesha mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa sababu hawajasema kama maombi hayo yanahusu mashahidi wote 15 pamoja na mambo mengine.
Amesema mara ya mwisho walisema wana mashahidi 15 lakini je wote hao wanataka kufichwa? wangeleta mashahidi wengine basi, sidhani kama wenzetu wanania ya kuendelea na kesi hii.
Pamoja na mambo mengine, Wakili Kibatala amedai upande wa mashataka unataka kuficha mashahidi wao hasa mapolisi kwa sababu wanajua kuwa watakuja kuwagalagaza hapa mahakamani na haswa kwa sababu kesi inasikikizwa mubashara.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 16, 2025 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa Upande wa Jamuhuri
Katika kesi hiyo ilidaiwa Aprili 3,2025
katika shtaka la kwanza Lissu alichapisha taarifa
inayosema “Uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 wagombea wa CHADEMA walienguliwa kwa maelekezo ya Rais” wakati akijua sio kweli.
Katika shitaka la pili inadaiwa kuwa Aprili 3,2025 Lissu kupitia mtandao wa youtube alichapisha tarifa inayosema “Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi”
wakati akijua sio kweli.
Na shtaka la tatu aliendelea kudai kuwa Lissu alichapisha tarifa ya uongo kwa nia ya kupotosha umma kupitia
mtandao wa youtube inayosema “Majaji ni ma-CCM hawawezi kutenda haki wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa mahakama ya rufaa” wakati akijua tarifa hiyo ni uongo na inapotosha umma.