Na Seif Mangwangi, Arusha
KAMPUNI ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania kupitia taasisi yake ya vodacom Tanzania Foundation imetumia wiki ya Azaki 2025 kutoa elimu ya ujasiriamali, pamoja na matumizi sahihi ya fedha kwa wanawake wafanya biashara wadogo na kuwataka wanawake hao kutumia ujuzi huo kujipatia kipato na kukuza biashara zao.
Akizungumza na Michuzi Tv leo Juni4, 2025, Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald amesema wao kama wadhamini wakuu wa wiki ya Azaki mwaka huu2025, wameamua kutumia kauli mbiu ya wiki hiyo ya ” pathway to progress”, kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake na wasichana.
Amesema kuwa lengo la kuwapatia wajasiriamali wadogo mafunzo hayo ndani ya wiki ya Azaki ni kuwakwamua kiuchumi na kuendana na dira ya taifa ya maendeleo ya 2050 kwa maslahi mapana ya nchi.
“ Sisi Vodacom Tanzania Foundation tumeshirikiana na CEO Roundtable Tanzania na chuo cha uhasibu Arusha (IAA), kuwapa mafunzo wanawake wajasiriamali wadogo kupitia mradi wa think equal lead smart, jambo hili tunalifanya ili kuwakomboa wanawake na kuwajenga kiuchumi, “Amesema Sandra.
Mkuu wa kitengo cha sheria chuo cha uhasibu Arusha (IAA),Winifrida ngowi amesema kuwa chuo hicho kimekuwa kikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake kiuchumi kwa kuwapa ushauri wa kisheria katika biashara.
Theresia amesema chuo hicho kimekuwa kikiwapa wanawake elimu ya namna ya kujikwamua kiuchumi na namna ya kuendesha biashara kwa kufuata sheria ikiwemo namna ya ulipaji kodi kwa serikali pamoja na kufanya biashara kidigitali ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Teknolojia.
“Tumewaita wanawake wafanyabiashara ndogo ndogo hapa kuwafundisha namna ya kufanya biashara mtandao kwa kuwa dunia ya sasa imebadilika na tunaamini elimu hii ya fedha tunayowapa itawasaidia sana katika kukuza biashara zao,” amesema winifrida
Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo Dkt. Joel Nanauka amewaasa wanawake kuitumia elimu ya fedha hasa katika utunzaji wa fedha na kuweka akiba ikiwemo kuacha tabia ya kukopa mikopo yenye riba kubwa kiholela .
Amesema ili uweze kupata fedha na kujijenga kiuchumi ni lazima kuwa na nidhamu ya fedha ikiwemo kuepuka matumizi yasiyokuwa ya lazima lakini pia kuweka akiba kila mara.
“Tunawafundisha ni namna gani ya kukopa fedha za kufanyia biashara na namna ya kukuza biashara zao na kulipa mikopo hiyo bila kuyumba kiuchumi, lakini pia tunawafundisha nidhamu ya fedha,”amesema.
Aidha Dkt. Nanauka amewataka wanawake wajasiriamali kutambua kuwa biashara zipo nyingi hivyo wanapaswa kuwa wabunifu na kufanya biashara tofauti, kuwa na biidi ya kujifunza maarifa ya kibiashara na kuwa wabobevu katika maeneo ya biashara zao.
“Haijalishi biashara ni ndogo kiasi gani ila unapaswa kuwa mbunifu ili uwavutie wateja wako,”amesema
Dkt.Nanauka aliwasisitiza wanawake wafanyabiashara kuwa makini na kuangalia vigezo vya mkopo kabla ya kukopa fedha, pamoja na kutumia mikopo hiyo katika malengo yaliyokusudiwa ambayo yatawasaidia kupata faida kupitia mikopo hiyo.
Washiriki hao ikiwemo wanawake kutoka katika jamii ya kifugaji pamoja na vijana wamehitimisha mafunzo hayo kwa kupewa vyeti vinavyowatambua kama washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali.