Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amezindua rasmi kituo cha Polisi Ngwala chenye hadhi ya daraja la C kwaajili ya kutoa huduma kwa wananchi wa kata hiyo pamoja na viunga vyake, kituo hicho kimejengwa na kampuni ya Madini ya Mamba kilichopo kata ya Ngwala Wilaya ya Songwe na Mkoa wa Songwe.
Akizindua kituo hicho Juni 04, 2025 Mh. Mavunde ameeleza dhumuni ya kujenga kituo hicho ni kwa kuwa kutakuwa na muingiliano wa watu ikiwa ni pamoja na mzunguko wa fedha kuwa mkubwa katika eneo hilo kutokana na mradi huo wa uchimbaji wa madini adimu duniani kitokana na hivyo uhalifu utakuwepo katika eneo hilo hivyo kituo hicho kipo mahususi kusaidia kupunguza uhalifu ili shughuli za kiuchumi ziendelee kwa amani na kuweza kuwanufaisha wananchi wa kata hiyo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga ameishukuru kampuni hiyo kwa kujenga kituo hicho pia amewasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania lGP Camilus Wambura kwa kumpongeza Mh. Waziri wa Madini kwa kuzindua kituo hicho ikiwa ni pamoja na kuwashukuru wananchi wa kata hiyo na kuwaomba ushirikiano wa kuwa karibu na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu ili kata hiyo kuendelea kuwa salama.
“Jukumu letu kwa sasa ni kuleta askari kwenye kituo hiki, wananchi mnakaribishwa kutoa malalamiko yenu lakini pia nawaomba msiwe mbali na Polisi kwani kazi za Polisi si zetu peke yetu tunawategemea katika kukilinda kituo hiki ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za wahalifu ili ziweze kushughulikia kwa haraka kwa lengo la kutimiza ujengwaji wa kituo hiki” alisema Kamanda Senga.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Mgodi huo Ismail Diwani alisema kuwa lengo la kujenga kituo hicho ni kuendeleza ushirikiano na taasisi za Serikali kwa ajili ya kufikisha huduma kwa jamii hasa katika masuala ya elimu, afya na usalama ili jamii iendelee kuwa salama katika maendeleo ya uchumi wa taifa.