Na John Bukuku Dar es Salaam, Juni 5, 2025,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini katika kuboresha maisha ya watu wenye uhitaji, ikiwemo watoto wenye mahitaji maalum, kama sehemu ya juhudi za kujenga taifa lenye usawa na huruma.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Watoto wenye Mahitaji Maalum kilichopo Kitopeni, Bagamoyo – hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam – Rais Samia alisisitiza kuwa serikali iko bega kwa bega na Kanisa katika kuhakikisha kituo hicho kinakamilika na kuwa na huduma bora.
“Nashukuru na nawapongeza kwa jitihada zenu. Serikali itashirikiana nanyi katika kukamilisha ujenzi na uendeshaji wa kituo hiki muhimu. Tumeshatoa ahadi ya Sh milioni 100, na michango kutoka kwa wasaidizi wangu pia itafikisha jumla ya Sh milioni 250,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alieleza kuwa mchango huo si wa kifedha tu bali ni sehemu ya dhamira ya serikali katika kuboresha ustawi wa watoto wote, hasa wale walioko katika mazingira magumu. Alitoa wito kwa watanzania wote kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia kwa moyo, akisisitiza kwamba “kutoa ni moyo, si utajiri.”
Katika hotuba yake, Rais Samia alitoa pongezi kwa Kanisa kwa kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza miradi ya kijamii nchini kote. Alisema huduma kama vile kuwahudumia wenye njaa, wagonjwa, na watoto wenye changamoto mbalimbali ni kiini cha utumishi wa kweli wa dini.
“Nilimsikiliza Katibu Mkuu wa Dayosisi hii na ametaja mambo mengi mazuri mnayoyafanya kote nchini. Huo ndio utumishi wa kweli wa dini. Ni wajibu wetu kushirikiana kujenga jamii yenye maadili na huruma,” alieleza Rais Samia.
Aidha, Rais alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya utoaji elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum, ikiwa ni pamoja na kuongeza walimu, vifaa vya kufundishia na kuboresha miundombinu husika.
Alihitimisha kwa kuwataka wadau mbalimbali – wakiwemo mashirika ya kimataifa, jumuiya za kidini, wataalamu wa ndani na nje ya nchi, pamoja na wawekezaji – kushirikiana katika kufanikisha maendeleo ya kituo hicho, ili kiwe mfano wa kitaifa katika huduma kwa watoto wenye uhitaji maalum.
“Ninaamini kupitia ushirikiano huu, tunaweza kufanikisha lengo la kuwa na jamii jumuishi inayowajali wote, hasa wale wanaohitaji msaada zaidi,” alisema.