* Asema Nishati sio jambo la anasa bali ni hitaji la msingi kwa maisha ya kila siku.
*Tanzania inajenga mfumo wa Nishati endelevu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa usalama wa nishati ni nguzo muhimu katika uwepo wa usalama wa nchi, maendeleo endelevu, ustawi wa jamii na uhifadhi wa mazingira hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya kuzalisha nishati safi na ya uhakika.
Mhandisi Mramba amesema hayo Juni 6, 2025 wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Usalama wa Taifa (National Security Symposium 2025) uliofanyika jijini Arusha ambao umekutanisha wataalam wa sekta ya Nishati na Usalama.
“Nishati si jambo la anasa, ni hitaji la msingi kwa maisha ya kila Mtanzania na ni injini ya maendeleo ya taifa lolote, hivyo usalama wa nishati unapaswa kuangaliwa kama ajenda ya kimkakati ya ulinzi wa Taifa,” amesema Mhandisi Mramba
Ameeleza kuwa, Serikali ya Tanzania inaendelea na jitihada za kuhakikisha nchi inakuwa na nishati ya kutosha ambapo kwa sasa uwezo wa kufua umeme umefikia megawati 4,414.69 huku mahitaji ya juu zaidi ya umeme yakifikia megawati 2,316.42.
Amesema kuwa, kati ya megawati hizo, megawati 4,031.71 zinatoka kwenye gridi kuu ya taifa, megawati 243.42 zinazalishwa na sekta binafsi na megawati 52 zinatoka Zambia na Uganda.
“Mahitaji ya juu zaidi ya umeme nchini yamefikia megawati 2,316.42, huku kasi ya ukuaji wa mahitaji hayo ikikadiriwa kuwa kati ya asilimia 10 hadi 15 kila mwaka hivyo tunachukua hatua madhubuti kuhakikisha tuna mchanganyiko imara wa vyanzo vya nishati ili kupunguza utegemezi kwa chanzo kimoja na kuongeza uthabiti wa mfumo wetu,” Ameeleza Mhandisi Mramba
Mhandisi Mramba ameeleza kuwa Tanzania imeanza vizuri safari ya kujenga mfumo wa nishati endelevu ingawa bado kuna safari ndefu, akieleza kuwa kwa sasa wateja zaidi ya milioni 5.44 wameunganishwa na umeme, kiwango cha upatikanaji wa huduma ya umeme kimefikia asilimia 78.4 mwaka 2020 na kaya zilizounganishwa na umeme zikiwa asilimia 46.
Kuhusu umeme katika Bara la Afrika amesema kuwa zaidi ya watu milioni 600 hawajaunganishwa na huduma ya umeme hivyo unahitajika mwelekeo wa pamoja wa Bara zima kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya nishati safi, salama na nafuu.
Katika mkutano huo, Mhandisi Mramba ametoa angalizo kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili kwa usalama wa nishati akisema kuwa “uharibifu wa mazingira na ukame unaoathiri vyanzo vya maji ni tishio halisi, tusipowekeza kwenye mchanganyiko wa nishati na teknolojia mpya, tutakuwa hatarini kiusalama na kiuchumi.”
Hata hivyo amesema kuwa, kwa mwaka 2025 pekee, Dunia imewekeza Dola za Marekani trilioni 2.2 katika teknolojia safi za nishati, ikiwa ni mara mbili ya uwekezaji unaofanywa kwenye mafuta ya visukuku na hiyo ikionesha kuwa mwelekeo wa dunia sasa ni kuelekea kwenye uzalishaji wa nishati safi hivyo Tanzania haiwezi kubaki nyuma.
Mramba pia amesisitiza kuhusu ushirikiano wa kikanda kupitia miundombinu ya nishati inayounganisha nchi na nchi ili kuhakikisha kunakuwa na usalama wa nishati hata wakati wa changamoto.
Pia ametoa wito kwa sekta binafsi kuwekeza zaidi katika Sekta ya Nishati kupitia ubia na Serikali (PPP), akieleza kuwa Serikali peke yake haiwezi kukidhi mahitaji ya nchi hivyo inahitaji uwekezaji kutoka kwa kila mdau mwenye dhamira njema ya kujenga taifa lenye nishati ya uhakika.