Na Mwandishi Wetu
TANZANIA ni miongoni mwa nchi ambazo zinashiriki kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) yanayoendelea nchini Japan, ambapo pamoja na mambo mengine inatumia maonesho hayo kama fursa ya kudani vivutio mbalimbali vilivyopo nchini vikiwemo vya utalii, uwekezaji nchini
Hatua inayokana na maonesho hayo kujumuisha mataifa mengi ambayo yanashiriki maonesho hayo mamilioni watu duniani wanatarajiwa kuyatembelea na hivyo kuliwezesha Taifa letu kutangaza fursa zake mbalimbali.
Maonesho hayo yalianza tangu Aprili 13, 2025 na yanatarajia kumalizika Oktoba 13, 2025, hii ni mara ya pili kwa Japan (Osaka) kuwa mwenyeji wa maonesho hayo ya kimataifa, ambapo mara ya mwisho yalifanyika 1970 (EXPO 1970).
Katika maonesho ambayo yaliambatana na Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika nyanja za kidiplomasia, kiuchumi, kibiashara, kisiasa na kijamii umezidi kuimarika.
Waziri Mkuu alisema Watanzania wanatakiwa kutumia maonesho hayo kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini ili kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Japan na ulimwenguni kwa ujumla kuja kuwekeza nchini na hivyo kukuza uchumi na kuongeza upatikanaji wa ajira hususan kwa vijana.
Alisema kutokana na mabadiliko makubwa ya kiserayaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya uwekezaji na biashara ikiwemo … na kuondoa urasimu Watanzania hawana budi kutumia fursa hiyo kuvinadi vivutio vilivyo nchini.
Waziri Mkuu alisema Wajapan wameonesha kuvutiwa na bidhaa nyingi zinazotoka Tanzania zikiwemo chai, kahawa, ufuta, tumbaku, tingatinga, vinyago, katani, viungo kama karafuu pamoja na madini mbalimbali yanayopatikana nchini, ambapo mauzo ya biashara kati ya nchi hizo yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni saba mwaka 2023 hadi bilioni 37 kwa mwaka 2024.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na duniani kote waje kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya elimu, afya, miundombinu, nishati, kilimo, utalii kwani Tanzania imeweka mazingitra mazuri ya uwekezaji na pia ina amani na utulivu.
“…Tanzania licha ya kuwa na fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo ardhi yenye rutuba, amani na mazingira tulivu, pia ni kitovu cha biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kusini na Kati kwa kuwa inapakana na nchi saba ambazo ni Uganda, Rwanda, Burundi, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Zambia, Malawi na Msumbuji hivyo kuwawezesha wawekezaji kupata masoko ya uhakika katika mataifa hayo.”
Waziri Mkuu ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanziba wakiwemo Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi mbalimbali alisema Serikali ipo katika mchakato wa kuvifanyia maboresho viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Julius Nyerere maarufu sabasaba ili viwe na hadhi ya kimataifa na kuwezesha kufanyika mikutano na maonesho ya biashara ya kikanda na kimataifa.
Jumatatu, Mei 26, 2026), Mheshimiwa Majaliwa alishiriki katika kongamano la biashara, uwekezaji na utalii ambalo lilihusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na Japan, ambapo pamoja na mambo mengine alisema Serikali itaendeleza mikakati ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wa Mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Japan ili waweze kunufaika na fursa zilizopo katika mataifa hayo.
Alisema kuwa Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kushiriki katika makongamano mbalimbali ya kimataifa ambayo yamekuwa yakiwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji ili kuongeza tija kubwa kwenye masuala ya biashara na uwekezaji.
“Tumewaeleza wafanyabaishara na wawekezaji hawa wa Japan fursa ambazo zipo nchini, hii ni mara ya tatu tunakutana na wafanyabara na wawekezaji kutoka Japan, tayari tumeanza kuona manufaa ya makongamano haya kutokana na kuongezeka kwa biashara kati ya mataifa haya mawili.”
Waziri Mkuu amesema hadi Machi 2025 jumla ya makampuni 24 kutoka Japan yamewekeza nchini Tanzania katika miradi mbalimbali yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 42.70 nchini na kuwawezesha jumla ya Watanzania wapatao 1,182 kupata ajira.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema licha ya uwekezaji wa makampuni hayo, Serikali ya Tanzania imeendelea kunufaika na ushirikiano wake na Serikali ya Japan kwa kupata misaada katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na miundombinu.
Pia, Waziri Mkuu ameshuhudia utiaji saini wa hati sita za ushirikiano ikiwemo ya ushirikiano katika kuendeleza sekta ya mafuta baina ya Serikali ya Tanzania na Shirika la JGC la Japan, hati nyingine ni baina ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Axcel Afrika kwa ajili ya kukuza uwekezaji nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleimani Jafo alisema dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uwekezaji inazindi kufunguka hivyo amewaomba Watanzania kuhakikisha wanachangamkia fursa hizo kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na Taifa.
Alisema lengo la Serikali la kuendelea kutafuta fursa hizo za biashara, uwekezaji na utalii ni kukuza uchumi pamoja na kuwezesha upatikanaji wa ajira nchini, na kwamba kipaumbele kimewekwa katika sekta za biashara, miundombinu, utalii, uchumi wa buluu, uwekezaji kwa kuwa Japan imepiga hatua kubwa katika sekta hizo.
Dkt. Jafo alisema kipaumbele kingine ni kutafuta wawekezaji watakaoshirikiana nao katika kuendeleza sekta ya kilimo ili kuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga miundombinu ya kisasa, katika sekta ya madini ni kuoyaongezea thamani madini ya kimkakati.
Naye, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Omar Said Shaaban alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga katika kutumia fursa za uwekezaji zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Japan.
Waziri Shaaban alisema tayari Serikali hiyo imeshaanza utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya uwekezaji ikiwemo ujenzi wa mitaa ya viwanda ambapo mmoja umejengwa mtaa wa Duga Zuze visiwani Zanzibar pamoja na eneo la Chamanangwe visiwani Pemba.
Mbali na miradi ya ujenzi wa mitaa ya viwanda, pia Waziri Shaaban amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara Zanzibar wameandaa jarida linaloeleza fursa za uwekezaji Zanzibar ambalo limezinduliwa na Waziri Mkuu na kugawiwa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan.
Alisema eneo jingine ambalo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga kutafuta wawekezaji ni uchumi wa Buluu kupitia mazao ya bahari ikiwemo usindikaji wa samaki ili kuhakikisha unafanyika kisasa zaidi kwa faida ya wananchi na serikali.
MAKUBALIANO BIASHARA YA KABONI
Fursa nyingine kuwa ambayo Watanzania wanatakiwa kuichangamkia ni biashara ya kaboni, ambapo vizi karibuni Serikali ya Tanzania na Japan zimetia saini Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika mpango wa pamoja wa uwekezaji katika biashara hiyo ambayo itawezeshakampuni za nchi hizo mbili kuwekeza katika Biashara ya Kaboni nchini Tanzania.
Utiaji saini wa makubaliano hayo ulifanyika Mei 28, 2025 Tokyo, Japan ambapo upande wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni na Serikali ya Japan ikiongozwa na Waziri wa Mazingira, Mhe. Asao Keiichiro (Kei).
Waziri Masauni alisema makubaliano ya mashirikiano yaliyosainiwa yanalenga kuimarisha uhusiano kati ya Japan na Tanzania kwa maendeleo endelevu na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambayoyatapanua soko la Biashara ya Kaboni kutoka kwa wawekezaji wa Japan watakaowekeza katika miradi ya biashara ya hiyo itakayoibuliwa nchini.
Alisema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawataka wataalamu kutoka nchi hizo mbili kushirikiana ili kuhakikisha makubaliano hayo yanaenda katika hatua ya utekelezaji.
Tayari Serikali ya Tanzania imeimarisha uwezo wa kitaasisi na kisheria katika usimamizi wa Biashara ya Kaboni ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa kanuni za mwaka 2022 za kuratibu biashara ya Kaboni na imeshaanzisha Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira iliyofanyiwa marekebisho ya 2025.
Awali, Kamishina Jenerali wa World Expo Osaka 2025 kwa Tanzania na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis alisema kongamano hilo ambalo ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya World Expo Osaka 2025 linalenga kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Japan.
Mkurugenzi huyo alisema maeneo ambayo yamepewa kipaumbele katika kongamano hilo ni kwenye sekta ya nishati, madini, kilimo, huduma za kibenki, utalii, uwekezaji, afya ambapo wafanyabiashara wa Tanzania wanakutana na wafanyabiashara wa Japan kujadiliana namna ya kushirikiana katika kukuza biashara na uwekezaji.
Awali, Meneja Uenezi na Masoko wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Khamis Dunia alisema ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) yanayoendelea nchini Japan umeiwezesha mamlaka yao kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo Zanzibar.
Alisema mbali na maonesho hayo, pia kitendo cha kushiriki katika mikutano iliyomhusisha Waziri Mkuu pamoja na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Kijapan vilivyofanyika jijini Tokyo alipata fursa ya kuelezea vipaumbe vya uwekezaji vilivyopo Zanzibar ikiwemo uchumi wa buluu na utalii jambo ambalo liliwavutia wawekezaji hao ambao tayari baadhi yao wameonesha nia ya kuwekeza Zanzibar.