Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kila mwaka takribani akina mama milioni 2.4 hupata ujauzito na kati ya hao asilimia 85 hujifungulia hospitalini na kufanya ongezeko la watoto ambao wanahitaji uangalizi wa karibu kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za afya.
Waziri Mhagama ameyasema hayo leo Juni 09, 2025 wakati akipokea na kukabidhi Nepi (Softcare), katoni zaidi ya 1600 kwa watoto wachanga katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General) zilizotolewa na kampuni ya Doweicare Limited zenye thamani ya zaidi ya milioni 65.
“Katika makuzi watoto huwa na uwezo wa kutambua hali ya kutaka kujisaidia wafikapo umri wa miaka miwili hadi mitatu kwa wakati wa mchana, umri wa miaka mitano kwa wakati wa usiku, hivyo wale wenye umri mdogo zaidi Nepi hizi zitawasaidia,” amesema Waziri Mhagama
Amesema sekta ya afya nchini imepiga hatua kubwa ya upatikanaji wa vifaa pamoja na vifaa tiba kutokana na umahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuongeza vifaa vya uchunguzi wa magonjwa na kupunguza safari za kufuata huduma hizo nje ya nchi.
“Mafanikio yote ya sekta ya afya yamesababishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha katika ngazi zote, sasa hivi kila kituo kipo vizuri, tuna wataalamu wa kutosha na tuna ile programu ya madaktari wa Mama Samia imewafikia Watanzania wengi ambao wanaendelea kufaidika na programu hiyo,”amesema Waziri Mhagama.
Sambamba na hayo ameongeza kuwa, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha inazidi kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na kwa wakati kwa kununua dawa na vifaa tiba kuanzia ngazi ya msingi.
Katika hatua nyimgine, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza
kwakuwa gharama za kutibu magonjwa hayo ni kubwa na lazima yatibiwe na wataalam wenye ubingwa na bobezi ambapo Serikali imeendelea kusomesha wataalam hao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema anawashukuru Softcare kwa kuweza kuwafikia kina mama wa Mkoa wa Dodoma, na amefurahishwa kujua kuwa kampuni hiyo imethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na kwamba bidhaa zake ni nzuri kwa kina mama na watoto bila kuleta madhara ya kiafya.
Kwa upande wake, Balozi wa Softcare, Zari The Boss Lady, amewasihi kina mama kuendelea kutumia pedi za kampuni hiyo kwani zimetengenezwa kwa pamba halisi na ni rafiki kwa mama awapo kwenye siku zake. Kwa watoto wadogo pia ni rafiki na hazichubui, hivyo kumfanya mtoto kuwa huru wakati wote.