Mtuhumiwa James Mbapila, anayedaiwa kuchakachua mitungi ya gesi, akiwa chini ya ulinzi ofisini kwake, baada ya Askari wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kampuni ya Orxy Gas kufanya operesheni maalumu ya kuwakamata watuhumiwa, mtaa wa Libya, Dar es Salaam.
……….
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Mashariki imetoa wito kwa kampuni zote zinazojihusisha na biashara ya gesi ya kupikia kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha usalama wa mitungi ya gesi pamoja na kudhibiti vitendo vya uchakachuaji vinavyofanywa na watu wasio waaminifu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Kampuni ya Oryx Gas kufanya operesheni katika maeneo ya Kariakoo na Upanga, ambapo watu wanaodaiwa kuchakachua gesi walikamatwa, Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Mhandisi Nyirabu Musira, amesema hatua hiyo ni ya kupongezwa na ni wajibu wa kampuni zote kuhakikisha usalama wa mitungi pamoja na ujazo unaokidhi viwango vilivyowekwa.
“Natoa rai kwa kampuni zote za gesi ya kupikia kuendelea kushirikiana na EWURA katika kudhibiti mitungi yao, hasa ile yenye ujazo wa zaidi ya kilo 16, kwani mitungi hiyo ndiyo inayotumiwa mara kwa mara katika vitendo vya uchakachuaji. Kanuni ziko wazi kuwa ni jukumu la kampuni kuhakikisha mitungi yao inafuatiliwa kwa karibu,” amesema Mhandisi Musira.
Ameongeza kuwa EWURA inashirikiana na kampuni zinazotoa huduma za nishati safi ya kupikia katika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Kwa mujibu wa sheria, mtu anayebainika kufanya biashara ya gesi bila kufuata utaratibu au kuchakachua ujazo wa mitungi anaweza kutozwa faini ya Sh milioni 20 au kifungo cha hadi miaka mitatu jela, au adhabu zote kwa pamoja.
“Tumekuwa tukichukua hatua dhidi ya wale wanaokiuka taratibu, na hatua zilizochukuliwa na Oryx Gas pamoja na wadau wengine ni sehemu ya wajibu wao. Leseni tunazotoa zinawataka wahakikishe usalama wa mitungi na ujazo sahihi wa gesi,” amefafanua.
Aidha, ameeleza kuwa kanuni za usimamizi wa LPG zinazitaka kampuni zinazoingiza na kusambaza gesi nchini kuhakikisha wanajua mitungi yao inamilikiwa na kutumika vipi, sambamba na kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika katika mazingira salama na yaliyoidhinishwa.
“Wakati wa operesheni, kampuni hizo huwa na maafisa kutoka EWURA na Jeshi la Polisi, na kupitia ushirikiano huu tumeweza kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya uchakachuaji,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja Mauzo Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, Bw. Shaban Fundi, amesema kuwa wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara na wanaendelea kuomba ushirikiano kutoka kwa serikali na taasisi zake ili kuimarisha juhudi za kudhibiti uchakachuaji wa gesi.
“Tumekuwa tukihamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia, lakini pia tunataka kuona wananchi wanapata gesi yenye ujazo halisi. Hatufurahishwi na wale wanaofanya uchakachuaji, na ndiyo maana tumeanzisha operesheni hizi,” amesema Bw. Fundi.
Ameongeza kuwa mitungi inapojazwa au kutumiwa kinyume na taratibu inaweza kuhatarisha maisha ya watu na kukwamisha juhudi za uwekezaji na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi.
“Leo tumewakamata watu waliokuwa wakijihusisha na uchakachuaji wa gesi. Tutaendelea na juhudi hizi, lakini tunasisitiza kuwa hatuwezi kufanikisha haya peke yetu. Tunahitaji usaidizi kutoka EWURA, Wakala wa Vipimo, na Jeshi la Polisi ili kwa pamoja tukomeshe biashara hii haramu,” ameongeza.
Amesema kuwa vitendo hivyo vinawaathiri moja kwa moja watumiaji wa gesi, kwani mitungi huwa haijajazwa ipasavyo, na njia zinazotumika kujaza gesi si salama, hali inayoweza kusababisha ajali au madhara makubwa kwa watumiaji.
“Katika vituo vyetu vya kujazia gesi, tunafuata hatua madhubuti kuhakikisha usalama. Hawa wanaojihusisha na wizi huu hawazingatii viwango vyovyote vya usalama – jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya wananchi,” ameeleza.
Akitaja baadhi ya maeneo yanayokabiliwa na changamoto hizo, Bw. Fundi alitaja mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Mwanza kuwa ni miongoni mwa maeneo yenye watu wanaofanya biashara ya gesi kwa njia zisizokubalika.
Amesisitiza kuwa ni vyema wafanyabiashara wa gesi wakatumia njia halali na akabainisha kuwa Oryx Gas inawakaribisha wafanyabiashara wote wanaotaka kushirikiana nao kwa njia sahihi, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati salama na yenye ujazo halisi.