Na Mwandishi wetu – Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Mohamed Mchengerwa amesema kuwa kwa Mamlaka aliyopewa na kuwa mwenye dhamana katika Mamlaka hiyo tayari amekwisha saini notisi mbili za kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Ambapo Notisi hizo ni pamoja na notisi ya kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika mamlaka za Wilaya ya mwaka 2025,na notisi ya kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka za Miji ya mwaka 2025.
Waziri Mchengerwa amesema hayo leo Juni 15,2025 jijini Dodoma wakati akitoa Tamko la kuvunjwa kwa Mabaraza na Mikutano ya Kamati za kudumu za Halmashauri kufikia Juni 20,2025 ambayo ni siku 7 kabla kwa kuvunjwa kwa Bunge ikiwa ni kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288, kifungu cha 84A, na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, kifungu cha 178A.
Ambapo amesema kuwa Notisi hizo zinatarajiwa kuchapishwa katika Gazeti la Serikali hivi karibuni, na zinabainisha kuwa vikao vyote vya Halmashauri pamoja na Kamati zake lazima vikome kufikia hiyo Juni 20,2025 ikiwa ni siku saba kabla ya kuvunjwa rasmi kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo linatarajiwa kuvunjwa tarehe 27 Juni, 2025 na Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan.
“Kwa kuzingatia Mamlaka niliyopewa na nikiwa Waziri mwenye dhamana kwa mujibu wa Sheria tayari nimekwisha saini notisi mbili zinazohusu kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”.
“Kufanyika kwa kikao chochote cha Halmashauri au Kamati zake baada ya tarehe 20 Juni ni kinyume cha Sheria na Notisi hizi, na Mtendaji Mkuu wa Halmashauri (Mkurugenzi) atawajibika moja kwa moja kwa ukiukwaji huo”.
Aidha amesema kuwa masuala yote ya kiutendaji katika Halmashauri yatasimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye atakuwa ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri katika kipindi hiki cha mpito huku akisaidiwa na wakuu wa Idara kama wajumbe wa Kamati.
Na kuongeza kuwa katika kipindi hiki hakutakuwa na uanzishaji wa miradi mipya au uwekezaji wowote mpya kwani haitaruhusiwa kubadili wala kurekebisha miradi, maamuzi au uwekezaji uliopitishwa kabla ya kuvunjwa kwa Mabaraza.
Ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri atawasilisha taarifa ya mwenendo wa menejimenti na maamuzi yote yaliyofanyika kwenye kikao cha kwanza cha Baraza jipya la Madiwani baada ya uchaguzi.
Pia Waziri huyo wa TAMISEMI ametumia Wasaa huo kutoa wito kwa wananchi wote, viongozi wa serikali, na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kushiriki kikamilifu katika kipindi hiki kwa kuzingatia misingi ya Utawala Bora, Maadili ya Utumishi wa Umma na kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.