Na WAF – Bariadi, Simiyu
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amezitaka Hospitali zote nchini kuwa na utamaduni wa kusimamia na kulinda miundombinu iliyopo kwa wivu mkubwa kwakuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu na vifaa tiba.
Waziri Mhagama amesema hayo leo Juni 15, 2025 alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simuyu kwa lengo la kukagua ubora na huduma zinazotolewa, kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya mama na mtoto, kukagua ujenzi unaoendelea katika jengo hilo pamoja na kuzungumza na watumishi katika hospitali hiyo.
“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameirahisisha sana kazi yetu ya tiba nchini, ameifanya iwe nyepesi, kuna mashine na miundombinu ya kila aina, hapo mtoaji huduma amerahisishiwa kwa kiasi kikubwa sana, na hiyo ndio faida ya Serikali sikivu,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagma amesema Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 29 kwenye huduma za afya ambapo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 19.8 hivyo miundombinu iliyopo inapaswa kulindwa kwa wivu mkubwa.
“Ombi langu jingine kwenu ninyi watumishi mzingatie maadili katika utoaji wa huduma zenu, wakataeni wale wanaokwepa kiapo chao cha maadili na kujiingiza kwenye makosa ya jinai, tuzingatie viapo vyetu na kutoa huduma kwa utu na usiri mkubwa,” amesisitiza Waziri Mhagama.
Katika hatua nyingine, Waziri Mhagama ameitaka Idara ya TEHAMA kusimamia mwenendo mzima wa usimamizi wa shughuli zote za hospitali na kuacha mara moja mapungufu yote yaliyopo katika Idara hiyo.
Jambo jingine, Waziri Mhagama amesema kumekuwa na tatizo la lishe katika mkoa wa Simiyu, ameielekeza hospitali kushirikiana na mkoa kutengeneza mazingira mazuri ya kutoa elimu kwa kina mama badala ya kusubiri hadi watoto wakiwa wagonjwa ili kuhakikisha vifo vyao vinapungua nchini.