Benki ya Standard Chartered Tanzania kwa kushirikiana na taasisi ya NIPE FAGIO wamefanya zoezi la usafi katika fukwe za Rungwe Beach, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuweka mazingira safi na salama katika fukwe za bahari.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Masoko na Chapa wa Standard Chartered, Bi. Desideria Mwegelo alisema kuwa kila mwaka kuelekea siku hiyo muhimu, benki hiyo imejenga utamaduni wa kufanya usafi wa fukwe kwa kushirikiana na familia pamoja na ndugu wa wafanyakazi wao.
“Tunalenga si tu kufanya usafi bali pia kutoa mafunzo kuhusu uhifadhi wa mazingira kwa jamii, ili kuhamasisha mabadiliko ya kitabia na kujenga kizazi kinachojali mazingira,” alisema Bi. Mwegelo.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii kubadili tabia na kuacha kutupa taka ovyo ovyo, hasa kwenye maeneo ya wazi kama barabarani na fukweni.
“Kama umenunua bidhaa kama ice cream, usitupe nje ya gari – iweke ndani hadi uifikie sehemu sahihi ya kutupia taka. Watoto wetu watajifunza kutoka kwetu,” aliongeza.
Aidha, aliwahimiza wadau mbalimbali wa mazingira na taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa kuanzisha na kuendeleza utaratibu wa kufanya usafi na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza mazingira.
Kwa mujibu wa Standard Chartered, ushirikiano wao na NIPE FAGIO umelenga kufanya usafi katika maeneo ya fukwe yaliyoathirika zaidi kwa uchafuzi, ili kuibua ari ya pamoja ya kutunza mazingira na kupunguza athari za taka baharini.


