*Airtel, NEMC waungana kulinda mazingira
Airtel, NEMC na wadau wa mazingira waungana kutokomeza taka plastiki
Dar es Salaam, Juni 13, 2025 – Kampuni ya Airtel Tanzania wakishirikiana na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) wameungana katika zoezi la pamoja la kulinda mazingira kwa kutokomeza taka za plastiki katika miji yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kwa kuhamasisha umuhimu wa kulinda mazingira pamoja na kufanya usafi kwenye fukwe za bahari.
Airtel Tanzania ilidhihirisha dhamira hiyo kupitia kugawa vifaa vya usafi pamoja na kushiriki kufanya usafi wa fukwe za bahari kwa kushirikiana na maafisa wa serikali, wafanyakazi wa Airtel, maafisa kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na wakazi wa mtaa wa Mbezi Beach B, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya serikali, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi Beach B, Asha Vionatis aliipongeza Airtel Tanzania kwa kuonesha mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa wajibu wa kampuni kwa jamii kwenye masuala ya mazingira, na kuihimiza kampuni hiyo kuendeleza juhudi hizo angalau mara moja kwa mwezi ili kuhakikisha fukwe zinabaki safi na salama dhidi ya uchafu wa plastiki.
“Uchafuzi unaotokana na plastiki ni miongoni mwa tishio kubwa kwa mfumo wa ikolojia ya bahari. Ni jambo la kutia moyo kuona kampuni kama Airtel inachukua hatua madhubuti kuelimisha jamii na kuhamasisha mabadiliko ya kweli kupitia utunzaji wa kimazingira,” alisema Vionatis.
Zoezi hilo la usafi lililofanyika katika Fukwe ya Kidimbwi, lilihusisha pia vipindi vifupi vya uelimishaji kuhusu utupaji sahihi wa taka, umuhimu wa matumizi bora ya mifumo ya uhifadhi wa taka, na athari za muda mrefu za plastiki kwa viumbe hai na mazingira kwa ujumla.
Kwa upande wake, akimwakilisha Kaimu Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Afisa Mazingira Mwandamizi, Bw. Jeremiah Nyakwaka, alitoa wito kwa wananchi, wawekezaji wanaofanya shughuli zao kando ya Bahari ya Hindi, pamoja na taasisi mbalimbali, kuhakikisha wanazingatia matumizi sahihi ya mifumo ya utupaji taka ili kuhifadhi mazingira.
“Natoa rai kwa kila mmoja wetu, katika kila kanda, kuhakikisha tunalinda na kuhifadhi mazingira ya fukwe zetu. Uchafuzi wa mazingira hauathiri viumbe pekee, bali hatimaye huathiri maisha yetu pia. Tumeendelea kutoa elimu mashuleni kuhusu utunzaji na ulinzi wa mazingira,” alisema Bw. Nyakwaka.
Kwa upande wa Airtel, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Udhibiti, Beatrice Singano, alisema kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kampuni hiyo katika kuunga mkono jitihada za kuhifadhi mazingira hapa nchini, akieleza kuwa uchafuzi wa mazingira unaotokana na plastiki ni miongoni mwa changamoto kubwa duniani.
“Kwa Airtel, tunaamini maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa bila kulinda mazingira. Usafi huu wa fukwe si tukio la mpito; ni tamko rasmi la dhamira yetu. Tumejidhatiti kuunga mkono ajenda ya taifa kuhusu uhifadhi wa mazingira,” alisisitiza Bi. Singano.
Kwa mujibu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), tani milioni 19 hadi 23 za taka za plastiki huingia katika mifumo ya maji kila mwaka na kuchafua maziwa, mito na bahari. Hili ni tatizo linalohitaji suluhisho la haraka na endelevu.
Aliongeza kuwa, kama kampuni inayoendesha huduma za mawasiliano na ubunifu wa kiteknolojia, Airtel Tanzania pia inatumia mfumo wake wa ujumbe mfupi wa simu kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na nafasi ya mazingira safi na salama katika maisha endelevu.
Zoezi hilo lilihitimishwa kwa Airtel Tanzania kutoa ahadi ya kuendelea kushirikiana na taasisi za serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kulinda na kuendeleza mazingira ya fukwe za bahari kupitia usafi, usalama na ustawi wa kudumu.