NA DENIS MLOWE IRINGA
WAZAZI na Walezi wametakiwa kuangalia matendo ambayo yako kinyume na utamaduni wa Kitanzania kwa kuwa ni moja ya vyanzo vikubwa ya makuzi ya watoto nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Fatma Rembo Organization’ ya mjini Iringa, ambaye pia Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Wanawake Taifa (UWT) na mjumbe wa baraza Kuu UWT mkoa wa Iringa, Fatma Rembo wakati akizungumza siku ya maadhimisho ya Mtoto wa Afrika Watoto iliyofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa.
Rembo alisema kuwa watoto wamekuwa wepesi kuiga matendo ya wazazi na walezi yaliyo mazuri na mabaya hivyo ni wakati ambao wanahitaji sana kuwa makini katika malezi ili kupata kizazi ambacho kina maadilli ya Kitanzania.
Alisema kuwa kuna baadhi ya wazazi walezi wanashindwa kuzingatia maadili ya kitanzania katika mambo mbalimbali kama mavazi yasiyo na stara, unywaji wa pombe hivyo kufanya watoto kuiga yale wanayoona kuliko kusikia.
Aliongeza kuwa maisha ya sasa yamebadilika sana walezi wamekuwa wakiichia nafasi kubwa kwa watoto kushinda wakiangalia luninga bila kutambua kwamba baadhi ya vipindi havizingatii maadili ya Kitanzania kitu ambacho kinamwaribu mtoto.
‘
‘Kutokana na wazazi wengi tuko bize sana kutafuta fedha, hivyo hatushindi na watoto nyumbani na tukirudi tunakuta wamelala, tukiulizia tu wanaendeleaje basi na asubuhi tutatoka tena mapema mtoto atashindwa kujua maadili yapoje kuna umuhimu wa kubadilika katika malezi” Alisema
Aliongeza kuwa kwa sasa watoto wanakumbana sana na ukatili na unaoongoza kufanyiwa watoto ni ukatili wa kingono ambao ni ubakaji na ulawiti ukatili huo mara nyingi unatokea ndani ya jamii, ambapo watoto wa kike ndio wanaoathirika zaidi hivyo muhimu jamii kuwa makini katika kuwalinda watoto na mambo hayo
Alisema kuwa matukio hayo ya kikatili yanasababishwa na uangalizi mdogo wa watoto, momonyoko wa maadili, visasi na imani za kishirikina na hii kwa kiasi kikubwa ukatili unasababishwa na wazazi kutokuzingatia au kufuatilia malezi ,makuzi na maendeleo ya watoto.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri ya UWT wanawake mkoa wa Iringa, Halima Mpinge ( Davina) alitoa rai kwa wasanii kuangalia maadili katika maisha wanayoishi na kuepuka baadhi ya mavazi ambayo watoto wamekuwa wakiiga kutokana na kuvutiwa nao pindi wanapowaona kwenye TV.
Alisema ifike wakati wasanii waangalie zaidi maadili yanayozangatia utamaduni wa Tanzania kuliko kuiga mambo ambayo watoto ndio mashabiki wao wakubwa hivyo kwa kuona wanasababisha kuiga na kuharibu kizazi kijacho kimaadili.
Fatma Rembo Organization ndio waliodhamini maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yanayofanyika kila mwaka Juni 16 kila mwaka ambapo pia halmashauri ya Manispaa ilimpatia Tuzo kwa mchango mkubwa aliotoa kwenye maadhimisho hayo kila mwaka.