Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akipokea vikundi vilivyoshiriki matembezi ya uhamasishaji kwenye Kituo cha Afya cha Kamabarage Manispaa ya Shinyanga kabla ya kushiriki zoezi la upandaji wa miti ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa Ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani leo tarehe 17 Juni, 2025. Kulia kwake ni Mkuu wa wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro na kushoto kwa ni Naibu katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis (katikati) akipanda mti aina ya mwembe katika Kituo cha Afya cha Kambarage Manispaa ya Shinyanga ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa Ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani leo tarehe 17 Juni, 2025. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Dkt. Paul Deogratius.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa Ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani yaliyofanyika leo tarehe 17 Juni, 2025 katika Manispaa ya Shinyanga.
Washiriki wakiwa katika Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa Ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani yaliyofanyika leo tarehe 17 Juni, 2025 katika Manispaa ya Shinyanga.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwa katika picha ya pamoja na viongozi pamoja na wadau wa usafi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa Ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani yaliyofanyika leo tarehe 17 Juni, 2025 katika Manispaa ya Shinyanga.
……
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa rai kwa wadau wa mazingira katika ngazi zote na wananchi kwa ujumla kuungana na Serikali kwa hali na mali katika mampambano dhidi ya kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Pia, amewaomba wananchi kuendelea kupanda miti na kuitunza ili kukabiliana na athari za ukame ambao unaathiri sekta mbalimbali ikiwemo maji, mifugo na kilimo ambazo zina umuhimu mkubwa kwa binadamu.
Ametoa wito huo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 17 Juni, 2025 katika Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza na viongozi na wananchi, Mhe. Khamis amesema pamoja na mambo mbalimbali Tanzania pamoja na jumuia za kimataifa kwa kushirikisha vizazi vilivyopo na vijavyo, imejitolea kuongoa hekta bilioni moja ya ardhi iliyoharibika kufikia mwaka 2030.
Alisema Tanzania ni moja ya waathirika wa hali ya ukame hivyo Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha inakabiliana na tatizo hilo kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikisha wizara za kisekta, taasisi za umma, washiriki wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi na taasisi za kidini.
Halikadhalika, Naibu Waziri Khamis alibainisha kuwa Serikali imeandaa Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame, imefanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Mazingira.
Kwa upande mwingine alisema Serikali imeendelea kuhakikisha kuwepo kwa ufugaji wenye tija pasipo kuharibu mazingira kwani ufugaji usiokuwa endelevu huchangia kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.
Akizungumzia siku hiyo alisema ina madhumuni ya kukuza uelewa miongoni mwa jamii juu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame na umuhimu wa utekelezaji wake duniani kote, hususan katika nchi zilizoathirika zaidi hasa Afrika.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuona umuhimu wa kuadhimisha siku hii mkoani humo.
Alisema kutokana na mkoa huo kukabiliwa na hali ya ukame hivyo ni jambo jema kuitumia siku hiyo kuhamasisha upandaji wa miti kuepuka changamoto ya kugeuka kuwa jangwa.
Mhe. Mtatiro alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza mkradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi ambayo si tu inasaidia katika utunzaji wa mazingira bali pia inachagiza uchumi.
Aliongeza kuwa mradi wa maji ya Ziwa Victoria kutoka mkoani Mwanza ni chachu ya zoezi la upandaji wa miti kwani unasaidia pamoja na matumizi mbalimbali lakini pia kuyatumia kumwagilia miti.
Maadhimisho haya yalikwenda sanjari na zoezi la upandaji wa miti katika Kituo cha Afya cha Kambarage kilichopo Manispaa ya Shinyanga na maadhimisho ya mwaka 2025 yanachagizwa na kaulimbiu ‘Ongoa Ardhi Kufungua Fursa’.