Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeshiriki katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yaliyozinduliwa rasmi jana juni 17, 2025 katika Viwanja vya Chinangali Park vilivyoko jijini Dodoma. Maadhimisho haya yanalenga kuelimisha wananchi kuhusu huduma za serikali, kutambua mchango wa watumishi wa umma, na kuhimiza mageuzi ya kiutendaji kupitia matumizi ya TEHAMA.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb), ambaye alisisitiza umuhimu wa maadhimisho haya katika kuhamasisha uwajibikaji, kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma za serikali, na kuwatambua watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi.
Waziri Simbachawene alieleza kuwa matumizi ya mifumo ya TEHAMA yameongeza ufanisi katika taasisi za umma, kurahisisha ufuatiliaji wa taarifa, na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Pia alihimiza taasisi zote kuhakikisha zinajiunga na mifumo hiyo ili kuhakikisha huduma zinapatikana kwa haraka na kwa uwazi zaidi.
TANAPA, kama taasisi ya serikali inayosimamia rasilimali za taifa imejizatiti katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA kama E-office, Microsoft navission(NAV) na mingineyo ambayo imeleta mageuzi makubwa ya kiutendaji. TANAPA imetumia jukwaa hilo kuonesha huduma zake kwa wananchi, kuelimisha kuhusu uhifadhi wa maliasili, kubainisha fursa za uwekezaji zinazopatikana pamoja na kuonesha mchango wa sekta ya utalii katika kukuza uchumi wa taifa.
Maadhimisho hayo yalianza rasmi tarehe 16 Juni na yanatarajiwa kufikia kilele chake tarehe 23 Juni 2025 huku yakibeba Kaulimbiu inayosema “Himiza matumizi ya mifumo ya kidigiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji.”