Naibu Katibu Mkuu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi (kushoto) akimkabidhi zawadi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika leo Juni 18, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS Prof. Appolinary Kamuhabwa akizungumza na waandishi wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika leo Juni 18, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.
Naibu Mkuu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi akizungumza na waandishi wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika leo Juni 18, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati akifungua Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika leo Juni 18, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.
Kaimu Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo MUHAS, Idara ya Tafiti na Ushauri wa Kiutaalamu Prof. Bruno Sunguya akizungumza na waandishi wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika leo Juni 18, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.
………………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka kuwekeza katika tafiti zenye kuleta tija kwa jamii pamoja na kuziwalisha kwa watunga sera ili ziweze kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Akizunguma leo Juni 18, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila.
Mhe. Majaliwa amesema kuwa kupitia machapisho wataweza kuishauri serikali na wadau wake namna bora ya kuongeza ushiriki wa wananchi katika vita dhidi ya magonjwa na kupambana na dhana potofu zinazoenezwa kwa kasi kwenye mitandao ya jamii.
Mhe. Majaliwa amesema kuwa wakati umefika kwa watafiti na watunga sera kuwekeza katika tafiti zenye kuleta tija kwa jamii, huku akieleza kuwa katika majadiliano ya kongamano hilo ni umuhimu wa kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini mahitaji halisi ya kujenga uwezo wa uzalishaji wa ndani na kuyafikisha kwa ajili ya utekelezaji.
“Tunakipongeza MUHAS kwa maendeleo katika miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea, nimeelezwa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kampasi za Kigoma na hii ya Mloganzila pamoja na awamu ya pili ya mradi wa kituo cha umahiri cha magonjwa ya moyo na mishipa. Maendeleo haya yanaakisi jitihada za kupambana na tatizo kubwa la magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuboresha mifumo ya afya nchini” amesema Mhe. Majaliwa.
Amesema kuwa kongamano hilo liwe sehemu ya kutazama mafunzo, huduma, sera na miongozo ya teknolojia katika sekta ya afya, kwa kuweza kubainisha mapungufu na kutengeneza mapendekezo kwa serikali na taasisi zote zinazohusika.
“Muangalie ni namna gani tunaweza kuhakikisha mifumo yetu inayotumia teknolojia inawasiliana na ushiriki wa sekta binafsi na za umma unaongezeka ili kupeana uzoefu na hamasa” amesema Mhe. Majaliwa.
Akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Daniel Mushi, amesema kuwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali umechochewa na matokeo chanya ambayo MUHAS imekuwa ikionesha katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“Katika miaka ya hivi karibuni, Chuo hiki kimefanikiwa kuingia miongoni mwa vyuo vitano bora katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, ushahidi wa ubora wa mafunzo, tafiti zenye tija, na weledi wa hali ya juu wa wakufunzi wake” amesema Prof. Mushi.
Amesema kuwa tafiti za MUHAS zimechangia kwa kiwango kikubwa katika kuibua na kuimarisha miongozo, sera, na mipango inayotekelezwa katika sekta ya afya na elimu.
Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema kuwa ameishukuru serikali kwa jitihada za dhati ambazo zimewezesha kuungwa mkono na wadau mbalimbali wa maendeleo na hivyo kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayoleta mageuzi makubwa katika mazingira ya elimu ya juu na afya nchini.
Prof. Kamuhabwa amesema kuwa kauli mbiu ya Kongamano hilo ni : “Kubadili Mifumo ya Afya Afrika: Kuweka Kipaumbele katika bunifu na tafiti katika Kukabiliana na Changamoto Nyumbufu za Afya Duniani.”
Amesema kuwa kauli mbiu hiyo imechaguliwa kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha mifumo ya afya kwa kutumia ushahidi wa kisayansi, teknolojia bunifu, na ushirikiano wa sekta mbalimbali ili kukabiliana na changamoto mpya na endelevu kama vile milipuko ya magonjwa, mabadiliko ya tabianchi, na ongezeko la magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.
Amesema kuwa katika kongamano la mwaka huu kutakuwa na mawasilisho zaidi ya 200 ya tafiti ambayo yatafanywa kwa njia ya maongezi (Oral Presentations) na kwa njia ya mabango (Posters).
Prof. Kamuhabwa mawasilisho haya yatafanywa na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi ambapo jumla ya washiriki 218 kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Tanzania, Kenya, Marekani, Norway na Zambia watatoa mawasilisho ya tafiti .
“Kutakuwa na mawasilisho ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Magonjwa ya kuambukiza na usugu wa vimelea vya magonjwa, Afya ya Mama, Mtoto na Kijana, Tiba mbadala na tafiti za chanjo, Afya ya kinywa, macho, masikio, pua na koo, Akili mnemba, teknolojia na usalama na afya kazini, na Utafiti wa mifumo ya afya na afya jumuishi.” amesema Prof. Kamuhabwa.
Amesema kuwa kutakuwa na mawasilisho makuu mawili kitaaluma ambayo yatatolewa siku ya kwanza na siku ya pili, ambapo siku ya kwanza kutakuwa na wasilisho ambalo litakuwa na kichwa cha habari; Kubadili Mifumo ya Afya Afrika: Kuweka Kipaumbele kwa Bunifu na Tafiti kwa Kukabiliana na Changamoto Zinazobadilika za Afya Duniani” ambapo litatolewa na Dkt. Nyanda Elias kutoka taasisi ya Taifa ya Tafiti za Tiba ya Binadamu (yaani National Institute for Medical Research – NIMR).
“Wasilisho kuu la pili lina kichwa cha habari: “Kukabiliana na Uhalisia wa Magonjwa Mahututi Barani Afrika; Kuweka Kipaumbele kwa Mahitaji Muhimu ya Kujenga Mifumo Thabiti ya Afya.” ambalo itatolewa na Prof. Tim Baker na Dkt. Karima Khalid kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili” amesema Prof. Kamuhabwa.