Jeshi la Polisi kupitia Kituo cha Utaliii na Diplomasia Mkoa wa Arusha limetoa elimu ya usalama kwa watoa huduma ya malazi maarufu kwa jina la ‘Airbnb’ kwa watalii na wageni wanaofika mkoani humo.
Mkuu Kituo hicho, Mrakibu wa Polisi SP Waziri Tenga wakati akitoa elimu hiyo leo amesema lengo la kuwakutanisha wadau hao ni kuwapa elimu, kusikiliza changamoto za kiusalama zinazowakabili na kuona namna bora ya kuzitatua ili kuhakikisha wageni wanaofika mkoani humo wanakua salama.
SP Tenga amebainisha kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa kuzingatia msimu huu kuna ongezeko kubwa la watalii lakini pia uwepo wa mikutano inayofanyika mkoani humo hivyo ni muhimu kuimarisha mahusiano mazuri baina ya Jeshi la Polisi na watoa hao wa huduma.
Kwa upande wake Meneja wa Chuo cha Taifa cha Utalii tawi la Arusha Dkt. Masinda Masweta amewataka watoa huduma hao kujisajili ili waweze kutambuliwa na Serikali ambapo itasaidia kujua maeneo wanakaopatikana lakini pia kurahisisha kuwafikia pindi wageni wanapokutana na changamoto za kiusalama katika makazi hayo.
Nao baadhi ya watoa huduma hizo wameeleza kufurahishwa na elimu hiyo ambapo wamejifunza mambo mengi hasa katika kutatua changamoto zao kwa haraka zaidi.