*Asema maonesho ya SABASABA mwaka huu ni ya tofauti kwa kuwa hadi sasa washiriki zaidi ya 3000 wa ndani na nje wamethibitisha kushiriki.
*Abainisha kuwa maonesho hayo yameandaliwa kisasa na kidijitali zaidi
*Ataka wananchi kutumia fursa zinazotokana na maonesho hayo ya SABASABA 2025.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Juni 26, 2025 ametembelea na kukagua maandalizi ya maonesho ya SABASABA 2025 Temeke Jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika viwanja hivyo vya SABASABA RC Chalamila alipata wasaa wa kusikia taarifa fupi ya maandalizi ya maonyesho hayo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Bi Latifa Khamis na kisha kutembelea mabanda mbalimbali yaliyoko ndani ya viunga vya SABASABA.
RC Chalamila amepongeza maandalizi ya maonesho hayo ambapo amesema hadi sasa tayari washiriki wa ndani na nje zaidi ya 3000 wamethibitisha kushiriki ” hii ni fursa muhimu na fahari kwa Taifa letu maonesho hayo licha ya kuwa na faida kiuchumi kusaidia pia kuikuza Tanzania kidiplomasia vilevile kuitangaza nchi yetu” Alisema RC Chalamila
Aidha RC Chalamila amewataka watanzania hususani wakazi wa Dar es Salaam kutumia vizuri fursa za kiuchumi zinazotokana na maonesho ya SABASABA ili kujikwamua kiuchumi
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TanTrade Bi Latifa Khamis amesema maonesho ya mwaka huu ni tofauti na miaka mingine kwa kuwa yameandaliwa kidijitali zaidi kwa kuwa hata wakati wa kuomba ushiriki ilikuwa Online, ukataji Ticket pia mwaka huu mitandao mbalimbali ya simu itatumika kukata tickets vilevile kutakuwa na usafiri wa kuzunguka ndani wa kisasa kabisa ambao utatolewa na shirika la Posta, pia kutakuwa na kijiji cha burudani na kijiji cha michezo hivyo wananchi watarajie mambo mengi mazuri.
Mwisho RC Chalamila ameridhia ombi la usafiri wa mabasi ya Mwendokasi kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri kwa kipindi chote cha maonesho ya SABASABA 2025.