Serikali ya Tanzania na Umoja wa Viongozi wa Afrika wa Kupambana na Ugonjwa wa Malaria (African Leaders Malaria Alliance-ALMA) wamesaini Mkataba wa Uenyeji (Host Agreement) katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma Juni 28, 2025.
Uwekaji saini huo umefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Katibu Mtendaji wa ALMA, Bi. Joy Phumaphi kwa niaba ya taasisi hiyo.
Katika salamu zake, Waziri Kombo alisema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni kiashiria cha kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na ALMA na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano unaohitajika ili taasisi hiyo iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Waziri Kombo alipongeza uongozi wa taasisi ya ALMA kwa kazi kubwa wanayoifanya za kuongoza mikakati barani Afrika ya kupambana na ugonjwa wa Malaria. Alisema kupitia ALMA hatua kubwa zimepigwa za kuziwesha nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo kuhamasisha ukusanyaji wa rasilimali kwa ajili ya kugharamia mikakati ya kitaifa ya kupambana na Malaria. Mikakati hiyo ni pamoja na uanzishwaji wa Malaria Scorecards, Mabaraza ya Malaria na programu za kuchangia fedha.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa ALMA, Bi. Phumaphi aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kusema uwekaji saini wa mkataba huo umewezekana kwa sababu ya uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alisema Mkataba huo ni mwendelezo tu, lakini ALMA ipo nchini Tanzania tokea ilipoanzishwa mwaka 2009 wakati wa uongozi wa Rais wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye wakati huo alikuwa pia Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe ambaye pamoja na mambo mengine, alitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kupitia ushirikiano baina ya Serikali na ALMA kupitia mikakati mbalimbali kama vile Malaria scorecards na Mabaraza ya Malaria.