NA DENIS MLOWE
MJUMBE wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dk Tumain Msowoya amechukua fomu ya kuomba ateulewe kugombea ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa.
Msowoya amewasili katika Ofisi za UWT Mkoa wa Iringa saa 8.00 asubuhi ambapo Katibu wa UWT Mkoa huo Mary Mwansengo alimkabidbi fomu.
Akizungumza baada ya kupokea fomu hiyo, Msowoya amesema ametafakari na ameona anatosha kugombea nafasi hiyo.
“Tayari nimechukua fomu nimeomba kuteuliwa ili niwe miongoni mwa wagombea wa nafasi ya ubunge. Uongozi ni hekima, busara na uwezo hivyo nimetafakari na nimeona ninatosha,” amesema.
Msowoya amewahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa na sasa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa.
Kwenye jamii kupitia taasisi yake ya Msowoya Foundation amekuwa akipigania na kutetea haki za watoto, wanawake, watu wenye Ulemavu, wazee na makundi yote pembezoni.
Mwansengo alimkabidhi Msowoya fomu hiyo huku akiisoma ilivyoandikwa kama ilivyoandikwa ukurasa wa mbele.
“Nakukabidhi fomu ya kugombea nafasi ya uongozi kwenye dola kwa maana ya Ubunge wa Viti Maalum,” amesema.