NA DENIS MLOWE IRINGA
MDAU wa Maendeleo Aidan Damian Mlawa leo amechukua fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kilolo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) akieleza dhamira yake ya kuisaidia jamii na kuwa msaidizi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amesema ameleta mageuzi makubwa ya maendeleo nchini.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu Mlawa ameishukuru CCM kwa kuwapa nafasi makada wake kushiriki kwenye nafasi mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Ametoa pongezi kwa serikali ya awamu ya sita kwa mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali akisema Kilolo sasa inahitaji kasi zaidi ya maendeleo ili kuendana na mwelekeo wa taifa.
Ameeleza kuwa atatoa maelezo zaidi endapo chama chake kitampa ridhaa ya kuendelea na safari ya kugombea, lakini kwa sasa ametosheka kusema kuwa tayari ameanza rasmi mchakato wa kugombea ubunge wa Jimbo la Kilolo.
Aidan Mlawa amesisitiza kuwa yuko tayari kushirikiana na wananchi pamoja na serikali katika kuharakisha maendeleo endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mlawa ambaye amekuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika wilaya ya Kilolo amesisitiza ushirikiano kuwezesha maendeleo ya jimbo la Kilolo na nchi kwa ujumla.